Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Makamu wa Rais wa Tanzania Dokta Philip Isdor Mpango ameagiza kushughulikiwa kwa ulipwaji fidia katika kipindi cha miezi mitatu kwa wakazi wa Makambako mkoani Njombe waliopisha maeneo ya uwekezaji katika miradi ya umeme wa Upepo na Soko la Kimataifa.
Dokta Mpango ametoa agizo hilo kwa wizara za Nishati pamoja na Viwanda na biashara akiwa mjini Makambako katika ziara yake ya kikazi kufuatia kuwapo kwa Malalamiko ya muda mrefu ya wakazi hao wanaodai serikali zaidi ya shilingi Bilioni 5 walizopisha maeneo yao.
Awali mbunge wa jimbo la Makambako na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe Deo Sanga amesema wananchi wake wamekuwa na malalamiko ya fidia kwa muda mrefu jambo lililosimamisha uchumi kwa takribani mwaka wa 6 sasa.
Siku chache zilizopita kabla ya ziara ya Makamu wa Rais wakazi wa Makambako akiwemo Rehema Kisinga na Maneno Chatanda walipaza sauti zao kudai fidia za maeneo yao huku wengine wakitaka uthaminishaji uanze upya kutokana na thamani ya ardhi kupanda kila siku.
Malalamiko hayo yamemfanya Makamu wa Rais kutoa maagizo kwa Wizara husika kushughulikia ulipwaji wa fidia hizo ili kuondoa kero kwa Wananchi.
Makamu wa Rais Dokta Philip Mpango anaendelea na ziara yake ya Kikazi mkoani Ruvuma.
0 Comments