Na Fadhili Abdallah,Kigoma
UTEKELEZAJI duni wa miradi ya maendeleo inayofanyika katika wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma imemkera Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango ambapo ameiagiza kamati ya siasa ya CCM mkoa Kigoma kumpatia haraka taarifa ya miradi waliyotembelea na kukagua kwa mkoa Kigoma aipitie na kuchukua hatua.
Akizungumza wilayani Buhigwe akiwa kwenye siku ya tatu ya ziara ya kiserikali mkoani Kigoma Makamu wa Rais alisema kuwa anazo taarifa za baadhi ya miradi utekelezaji wake haifanani na fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi hiyo na kwamba hawezi kukubaliana na hali hiyo ni lazima waliosababisha hali hiyo wawajibishwe.
Dk.Mpango alitoa mfano wa soko la Kimataifa la Mnanira lililopo Mpakani na nchi ya Burundi alisema kuwa taarifa alizonazo kuhusu utekelezaji wa soko hilo uamridhishi na kutaka apatiwe taarifa nzima ya mradi huo na kutoa maagizo kwa Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma, Jamal Tamim na Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye kumpatia taarifa za miradi waliyokuwa wakitembelea na kukagua haraka ili aweze kuchukua hatua.
“Serikali imeleta fedha nyingi mkoani Kigoma kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kuleta maendeleo kwa wananchi lakini kuondoa kero na kuboresha maisha yao lakini kuna watu wamepewa mamlka ya kusimamia miradi hiyo wanafanya wanavyotaka wao na miradi haiku kwenye hali ambayo serikali inataka mingine ipo wilayani kwangu nilipozaliwa, hiyo haiwezekani lakini niondoke na kichwa cha mtu wanaofanya mcheo na miradi hiyo,”Alisema Makamu wa Rais.
Akizungumza katika mkutano huo kwenye hospitali ya wilaya ya Buhigwe Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa kwa mwaka wa fedha uliomalizika Juni Mwaka huu serikali imeleta mkoani Kigoma kiasi cha shilingi Bilioni 38.1 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundo mbinu ya afya ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 35.2 sawa na asilimia 92.4 zimeshatumika kwenye utekelezaji wa miradi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma,Jamal Tamim ameipongeza serikali kwa kutoa fedha nyingi kwa mkoa Kigoma na kutekeleza miradi ya kimkakati hivyo kupitia kamati ya siasa wako macho kuangalia utekelezaji wa miradi hiyo inatekelezwa kikamilifu kama ilivyopangwa na kwamba watatumia nafasi yao katika usimamizi wa ilani kutoa taarifa za hali ya miradi na kutoa taarifa kuhusu wasimamizi wasiotekeleza wajibu wao wawajibishwe.
0 Comments