Header Ads Widget

MAJI KUTOKA ZIWA VICTORIA YANUFAISHA WANANCHI IGUNGA

 


Na abdallah Amir-Matukio Daima, Igunga.

MRADI mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria umeanza kuwanufaisha wananchi 49,000 wa kata tatu za Wilaya ya Igunga mkoani Tabora.


Mradi huo ambao umegharimu Shilingi Bilioni 5.5 umejengwa na Kampuni ya Help Desk Engineering Limited ya nchini India  na umesaidia kupunguza adha kubwa ya wananchi ambayo walikuwa wakiipata wananchi kwa muda mrefu.


Akizungumza wakati wa ziara yake hivi karibuni, Mbunge wa Manonga Seifu Khamisi Gulamali (CCM) alisema Serikali imesikia kilio cha wananchi ambao kwa miaka mingi walikuwa wakitaabika kupata maji safi na salama na kusababisha kushindwa kufanya shughuli nyingi za kiuchumi kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji.


Mbunge huyo alisema Serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan imepanga kuyatoa maji hayo kutoka Kata ya Nkinga hadi Kata ya Nsimbo ambapo maeneo hayo yote yatanufaika na maji ya Ziwa Victoria.


Hata hivyo Mbunge Gulamali alisema amesikitishwa na kuwapo kwa kikundi kidogo ambacho kimekuwa kikimchonganisha na  wananchi wa Kata ya Ndembezi.


“Kikundi hicho kimekuwa kikiwambia wananchi kuwa mimi nimewatenga wapiga kura wangu wa Kata ya Ndembezi wakati si kweli na ndiyo maana hata maji yameweza kufika kwenye kata hiyo".


“Hivyo niwaombe  Wana Ndembezi na maeneo mengine ya jimbo hili la Manonga kukipuuza kikundi hicho na badala yake muendelee kuiamini Serikali yenu kwani imejipanga kumtua ndoo mama kichwani.”alisisitiza Mbunge Gulamali.


Aidha baadhi ya wananchi wa kata za Ndembezi, Ugaka na Nkinga Mwanahamisi Iddi, Mrisho Njile, Ramadhani Mussa na Isebelo Kinyongwa kwa nyakati tofauti walisema kabla ya mradi huo wa ziwa Victoria walikuwa wakifuata maji ya mito ambayo hayakuwa safi na salama kutoka sehemu mbalimbali.


Mwanahamisi alisema “katika maeneo hayo tulikuwa tunakumbana na wanyama kama fisi, kubakwa pamoja na kupigwa na waume zetu pindi tunapochelewa kuwahi nyumbani”alisema


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ndembezi Otto Humbi Mayonga (CCM) alisema kabla ya mradi huo kufika kwenye kata hizo tatu wananchi walikuwa wakipata shida kubwa ya kufuata maji umbali mrefu huku wakikumbana na wanyama hatarishi wakiwemo fisi, hivyo aliishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kufikisha maji katika kata hiyo.


Mwakilishi wa mamlaka ya maji kutoka RUWASA Wilaya ya Igunga, Adam Ngakonda alisema mradi huo wa maji kutoka ziwa Victoria hadi Igunga  Serikali ilitoa tena  Bilioni 5.5 kwa ajili ya kutoa maji kata ya ziba hadi kata ya Nkinga iliyopo Hospitali ya rufaa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI