Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkuu wa wilaya Kigoma Salum Kalli amekemea tabia ya wahudumu wa mabasi ya abiria yanayofanya safari nje ya mkoa kuwatelekeza abiria na kukimbia magari yao yanapopata hitilafu ambapo ametaka tabia hiyo iachwe mara moja.
Kalli alisema hayo alipoitisha mkutano wa dharula na makodakta na wasimamizi wa magari hayo katika kituo kikuu cha mabasi mjini Kigoma kufuatia kukithiri kwa vitendo vya wafanyakazsi hao kukimbilia abiria kwa siku za karibu.
Kutokana na hilo Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wasimamizi hao wa magari ya abiria kufuata taratibu za leseni zao kwani kinyume chake sheria ya usafirishaji itafuatwa na magari hayo kufungiwa na kufutiwa leseni
Hata hivyo alisema kuwa anatarajia kuwa na kikao na wamiliki wa mabasi yote ya abiria mkoani humo kuzungumzia changamoto zinazojitokeza ili kuwezesha usafirishaji unaofanyika usiwe na kero na usumbufu kwa abiria.
Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa usalama barabarani wilaya ya Kigoma Ibrahim Mbarouk alisema kuwa wameimarisha ukaguzi na usimamizi wa sheria na taratibu za usalama barabarani na usafirishaji abiria ili kuhakikisha abiria wanasafiri kwa kadri ya ratiba zilizowekwa na kwamba wameshaanza kuchukua hatua kutokana na changamoto zilizojitokeza kwa siku za karibuni.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha wasafirishaji abiria mkoa Kigoma (KIBOA), Almasi Juma alisema kuwa amesikia maelekezo ya Mkuu ya na kwamba watachukua hatua kuboresha taratibu za usafirishaji ili kuondoa usumbufu kwa abiria.
0 Comments