Header Ads Widget

RHMT NA CHMT SIMAMIENI MIRADI YA AFYA – DKT. MFAUME

Mkurugenzi wa Idara ya Afya Lishe na Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais TAMISEMI  Dkt. Rashid Mfaume  amezielekeza timu za usimamizi wa afya ngazi za Mikoa (RHMT) na ngazi za Halmashauri (CHMT) na timu za usimamizi wa vituo vya afya kusimamia miradi ya afya inayotekelezwa katika maeneo yao Kwa ukaribu zaidi.

Dkt. Mfaume amesema hayo wakati wa majumuisho ya Mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya ziara yake ya Usimamizi shirikikishi ya  upatikanaji wa huduma za afya, Lishe na Ustawi wa Jamii katika mkoa huo.

“Mara nyingi RHMT na CHMT tumekuwa tukichelewa sana kujishirikisha na miradi, jengo likianza hadi kukamilika hatujatembelea kulikagua wakati sisi ndio wataalamu na  watumiaji wakubwa wa majengo hayo” amesema Dkt. Mfaume

Amesema kutokana na timu hizo kutofatilia miradi hiyo kwa ukaribu imesababisha miradi mingi kutekelezwa kinyume na Miongozo na maelekezo ya maeneo ya utoaji wa huduma za afya yanavyotakiwa kuwa.

“Kutokana na miongozo yetu, majengo yanajengwa na kuna viwango vyake katika kila eneo  kama na maabara n.k, na yanafuatana toka mgonjwa anaingia eneo la kupata huduma (OPD) hadi katika maeneo ya kufulia na vichomea taka hivyo nahimiza kujishirikisha na kutoa ushauri wa kitaalam kwa mafundi wetu” amesisitiza

 Aidha, Dkt. Mfaume amezitaka Halmashauri kuhakikisha majengo mbalimbali ya kutolea huduma za afya ambayo yamekwisha kukamilika kuanza kutoa  huduma kwa wakati kwa lengo la kuwahudumia wananchi kama ambavyo Serikali imekusudia.

Pia amezitaka Halmashauri kuendelea kuajiri watumishi kwa mkataba ili kuendelea kupunguza uhaba wa watumishi katika maeneo ya kutolea huduma za afya, hasa katika maeneo yenye watumishi wachache.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Aman Mafuru amesema ziara hiyo ya Mkurugenzi imekuwa kama jicho la wazi la kujitathmini kama Mkoa kwa namna unavyotekeleza majukumu yake katika Sekta ya afya. 

“Katika ziara hii ya usimamizi yapo mambo mengi umeyaona na kutolea maelekezo na tayari sisi kama Mkoa tumeanza katika baadhi ya maeneo na tunaendelea kwa yale bado”.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI