NA HADIJA OMARY LINDI.......
Mtoto wa miaka 9 aliefahamika kwa jina la Yusufu Salumu mkazi wa Rutamba Manispaa ya Lindi amefariki dunia baada ya kuchomwa moto mgongoni wakati akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa degedege na mganga wa kienyeji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi kupitia kamanda wa jeshi hilo Mkoa wa Lindi , ACP Pilly Mande alisema mnamo tarehe 01/07/2023 katika kijiji cha Rutamba wilaya ya Lindi, Marehemu alipelekwa na wazazi wake nyumbani kwa mganga wa kienyeji aliyefahamika kwa Jalina Juma, 45 kwa lengo la kupatiwa matibabu ya ugonjwa wa Degedege uliokuwa unamsumbua
Alisema Baada ya kumfikisha mganga huyo aliahidi kumtibu na ndipo alipomlaza chali kwenye kitanda ambacho hakikuwa na godoro na kisha chini aliweka nyasi na kuziwasha moto uliopelekea kumuunguza sehemu za mgongoni na kumsababishia majeraha makubwa.
Alisema baada ya tukio hilo mtoto huyo alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Lindi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambapo umauti umemkuta tarehe 08/07/2023 akiwa bado Hospitalini hapo .
Polisi walipata taarifa hizo na kufika nyumbani kwa mganga huyo ambapo alifikishwa kwenye kituo cha Polisi kwa mahijiano
Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu ili shughuli za mazishi ziendelee.
0 Comments