MBUNGE wa Jimbo la Moshi vijijini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, Prof. Patrick Ndakidemi amewataka wasomi nchini kujiunga katika siasa na kutumia Elimu yao kuisaidia jamii katika kukuza maendeleo.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana katika mahafali ya wanafunzi wa Chama cha Mapinduzi vyuo na vyuo vikuu wilaya Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo alisema kuwa, wapo baadhi ya wasome ambao wamekuwa wakidhani kuchanganya siasa na Elimu sio vizuri.
"Wasomi wenzangu niwaeleze tu ukweli siasa inalipa hivyo ninyi kama wasomi jiungeni kwenye siasa ili tuweze kupata viongozi wasomi watakaotumia Elimu yao kuisaidia jamii na kuwaletea maendeleo" alisema Mbunge Prof. Ndakidemi.
Mbunge huyo alisema kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasani imeonyesha dhamira ya dhati katika kuinua Elimu nchini hii ni baada ya kutoa elimu bila malipo kuanzia awali mpaka kidato cha sita sasa kwa mwaka huu wa fedha wanafunzi wa vyuo vya kati wanaenda kupata mikopo na watakaopangiwa vyuo vya ufundi hawatalipa ada Serikali imewalipia.
"Niwasihi ninyi vijana wasomi mtakaporejea majumbani mwenu wahamasisheni wadogo zenu kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao kwani kwa sasa hakuna kikwanzo kitakachowafanya kushindwa kutimiza ndoto zao" alisema Prof. Ndakidemi.
Aidha Mbunge huyo aliiomba Serikali kutenga eneo katika wilaya ya Moshi ili yeye Mbunge aweze kuleta mradi wa Kilimo wa BBT utakaosaidia vijana kujiajiri.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo aliwaomba vijana kuendelea kukiunga mkono chama cha Mapinduzi ili kiendelee kushika Dola na kuwatumikia wananchi wote bila kujali Itikadi ya vyama vyao.
Mwisho...
0 Comments