Na,Jusline Marco;Arusha
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Meru, Eliasi Kitoi Nasari amewataka wazazi kulisaidia kanisa katika kujenga maadili mema kwa watoto wao kwa kuwaombea kusudi kuweza kuwa na kizazi chenye maadili mema na hofu ya Mungu.
Askofu Kitoi ametoa rai hiyo katika ibada ya kumsimika Mkuu wa Jimbo la Magharibi Mteule Mch.Franael Isangya na Makamu Mkuu wa Jimbo Mteule Mch.Emmanuel Mbise ibada iliyofanyika kwenye Kanisa la KKKT Usharika wa Akeri Wilayani Arumeru.
Aidha amesema kuwa mporomoko wa maadili ni wimbi la wakati huu ambalo liko kwa madhehebu na makanisa yote ambapo amewataka viongozi wa dini wakiwemo wachungaji kupaza sauti zao na kusema ukweli katika kukemea vitendo viovu ili jamii iweze kuwa salama.
Awali akimsimika Mkuu huyo wa Jimbo,Askofu Kitoi amemtaka kusikiliza na kutii ahadi na maonyo ya neno la Mungu katika kumtumikia Mungu na kuliongoza Kanisa na kuwataka viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele katika kikemea maovu na kuliongoza kanisa kwenye njia iliyo njema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Meru Hezron Mbise katika ibada hiyo amewasihi viongozi hao wa dini kutumia nafasi zao kukemea vitendo vya ushoga vilivyoibuka katikati ya jamii huku akisema kuwa mpango wa shetani ni kuiharibu jamii na taifa kwa ujumla.
Naye Mkuu wa Jimbo la Magharibi Mch.Franael Isangya akizungumza mara baada ya ibada hiyo ameahidi kuwatumikia wakristo na Jimbo kwa ujumla ikiwemo kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Pamoja na hayo Mkuu wa Jimbo la Zanzibar DMP-mch.Shukuru Maloda amewataka watumishi wa mungu kwa nafasi zao kuwafundisha waumini wao habari ya maombi na wakati wote kutafuta kulijua neno la Mungu kutoka na uchaji wa maombi kupungua kwa wakristo.
0 Comments