Beng'i Issa Katibu Mtendaji wa baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC) akizungumza katika ufunguzi wa maonyesho ya sita ya mifuko na program za uwezeshaji wananchi kiuchumi yanayofanyika mjini Kigoma
(Picha na Fadhili Abdallah)
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amesema kuwa maonyesho ya sita ya mifuko na program ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yataongeza chachu kwa watu mbalimbali mkoani humo kupata habari na taarifa ambazo zitasaidia kuimarisha shughuli zao za uzalishaji na uwekezaji.
Andengenye alisema hayo akifungua maonyesho hayo yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwanga Community Centre mjini Kigoma na kusema kuwa mifuko hiyo ni muhimu kwa wazalishaji na wawekezaji kupata taarifa za fursa zinazopatikana kwenye mifuko hiyo ikiwemo mikopo na uwezeshaji.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya Kigoma,Salum Kalli alisema kuwa Kigoma ni mkoa wa kimkakati kiuchumi na hivyo maonyesho hayo yamekuja wakati muafaka kwani yatatoa mwanga namna ambavyo wazalishaji na wawekezaji wanaweza kufanya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi ikiwemo biashara na shughuli za viwanda.
“kwenye maonyesho haya zipo taasisi zinazosimamia mikopo, zinazosimamia uwezeshaji na uwekezaji,taasisi zinazosimamia dhamana kwenye mikopo ya mabenki, taasisi za kusimamia ubora na namna ya kufanya biashara za kuvuka mpaka,masoko na Ithibati ambapo kwa mkoa Kigoma ni fursa kubwa sana kuwa na taarifa kuhusu utendaji wa taasisi hizo,”Alisema Mkuu huyo wa mkoa.
Awali Katibu Mtendaji wa baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC), Beng’I Issa alisema kuwa katika maonyesho hayo mifuko ya uwezeshaji, taasisi zinazotoa mikopo, mabenki na taasisi zinazosimamia biashara na uwekezaji zimeshiriki kukiwa na jumla ya mifuko na program za uwezeshaji 72 nchini ambayo inasaidia katika kutekeleza mpango huo.
Issa alisema kuwa hadi kufikia mwezi machi mwaka huu mifuko na program hizo za uwezeshaji zimewezesha kutolewa kwa mikopo yenye thamani ya shilingi Trilion 6.1 kwa wajasiliamali milioni 8.6 kati yao wajasiliamali wanawake wakiwa ni milioni 4.7 na wanaume milioni 3.9 na kutengeneza ajira milioni 17.6.
Akizungumza katika maonyesho hayo Afisa Habari na mawasiliano wa Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA), Christina Njovu alisema kuwa ni jambo muhimu kwa wajasiliamali kusajili majina ya biashara zao na kampuni ziweze kutambulika ndani na nje ya nchi kwa urahisi.
Njovu alisema kuwa BRELA inasajili leseni kundi A ambazo kiasi kikubwa zinahusu wafanyabiashara wanaofanya biashara za kuvuka mpaka hivyo wajasiliamali na wafanyabiashara wa mkoa Kigoma ambao wako mpakani itawapa nafasi nzuri ya kufanya biashara ya kuvuka mpaka na nchi jirani za Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo na Burundi.
0 Comments