Header Ads Widget

MTUHUMIWA MAUAJI YA MKE WAKE, AMTUMIA SMS MAMA MKWE





Mtuhumiwa anayesakwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za mauaji ya mkewe, amemwandikia mama mkwe ujumbe mfupi (SMS), kuelezea ushiriki wake katika tukio hilo.


Mtuhumiwa anadaiwa kutuma ujumbe huo wakati polisi wakiwa tayari wamechukua sampuli kwa ajili ya kupima vinasaba (DNA) ili kuthibitisha kama mwili uliokutwa umeteketea kwa moto Februari 19, 2023 ni wa Josephine Mngara (27).


Mwili wa mwanamke huyo ulikutwa umeteketea kwa moto kwenye nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika (pagale) ambapo kulikutwa pia michirizi ya damu kutoka kwenye nyumba ya mkazi wa eneo hilo.



Katika ujumbe huo aliomtumia mama mzazi wa marehemu, Theodora Msuya, mtuhumiwa anadaiwa kusema roho inamuuma kwa tukio lililofanyika. Mwanamume huyo ambaye jina limehifadhiwa ndiye alikuwa akiishi na marehemu.


Akizungumza na gazeti hili jana, Msuya alisema katika sms aliyotumiwa, mtuhumiwa alielezea nini kilitokea siku hiyo na kwamba alimkuta mwanamume mwingine na mkewe na ukatokea ugomvi na ametaja jina la mtu anayedai ndiye muuaji.


SMS hiyo iliyohaririwa inasomeka “Mama samahani si kosa langu, nilimkuta (anamtaja) na mke wangu kwangu, nikavunja mlango tukaanza kupigana. Mimi nikashika panga na yeye akachukua mpini wa jembe.


“Akawa anarusha nikakwepa ndo akampiga mke wangu mpaka chini. Akanipa nauli akaniambia sepa niachie mimi... Muulize (anamtaja), mama mimi sijui roho yangu inauma sana mchana mwema.”


Mama wa binti huyo, alidai kama waliotenda tukio hilo wamejitokeza na kuomba radhi, wanaliomba Jeshi la Polisi kuwapa mabaki ya mwili wa mtoto wao kwenda kuzika kwa kuwa ni muda wameweka msiba nyumbani bila kujua mwafaka. “Mpaka sasa hatujapewa mwafaka na Jeshi la Polisi juu ya kuzika na nini kinachoendelea, tumeweka msiba hapa nyumbani tuna zaidi ya wiki sasa, watu wamekaa hapa wameacha shughuli zao na familia zao wako hapa nyumbani.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI