NA, TITUS MWOMBEKI, KAGERA
BAADHI ya wadau wamendeleo na viongozi wa vijiji vinavyounda kata ya Kangabusharo na Karabagaine zilizopo wilaya ya Bukoba vijijini wamepongeza ushirikishwaji unaofanywa na viongozi wa mkoa kwa kushirikiana na uongozi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam ili kuwawezesha kutoa maoni yao juu ya mradi huo mkubwa.
Mwijilisti Audax Mulashani, mkazi wa kata Karabagaine wilaya Bukoba amesema kuwa wananchi pamoja na wadau wa maendeleo kutoka Kata ya Karabagaine na Kangabusharo ambapo chuo Cha Dar es Salaam tawi la Kagera kitajengwa wameshirikishwa vya kutosha kupitia mikutano ya kijiji na wamekubariana kwa pamoja na kutoa eneo bure ambalo litatumika kwa ujenzi wa chuo hicho.
"Viongozi wengi kuanzia wa ngazi ya chini hadi mkoa wamekua wakija hapa na tumefanya mikutano pia kwenye vijiji vyetu wakitushirikisha mambo mbalimbali yanayohusu mradi huu na faida zake na leo wamekuja viongozi kutoka chuo kikuu wametuambia tena faida za ujio wa chuo hiki lakini pia tumetoa maoni yetu, kwakweli hili ni jambo jema kwetu"
Aidha, wameiomba serikali kuhakikisha chuo hicho kinafundisha masomo kilimo na mifugo, ili kuwawezesha wananchi wa Wilaya ya Bukoba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla, kupata elimu hiyo ambayo itawasaidia kujiiua kiuchumi kupitia sekta hiyo pamoja na kuzingatia utoaji wa ajira kwa wazawa wa eneo hilo ili waweze kunufaika na ujio wa chuo hicho.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bukoba, Felister Shayo amewataka wananchi kutoweka vikwazo wakati wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chuo hicho, maana uwepo wake utasaidia kuinua uchumi wa wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla.
Naye, Dr. Dotto Kuhenga mkuu wa mawasiliano chuo kikuu cha Dar es Salaam na mtaalamu wa mawasiliano katika mradi wa The Higher Education for Economic Transformation(HEET) amewataka wanachi kuupokea mradi huo kwa mikono miwili na kuepuka sababu ambazo zinaweza kupelekea mradi huo kushindwa kutekelezwa mkoani Kagera.
"Ni vema kuwa tuupokee mradi huu kwa kutoa ushirikiano mkubwa unaohitajika kwani kwa kufanya hivyo tunaisaidia serikali kutekeleza mradi kama huu wa maendeleo kwa wakati, na sisi wananchi kuyapata manufaa yake kwa haraka na kwa tija kubwa" alisema Dkt. Kuhenga.
Aidha ameeleza faida za chuo hicho mkoani kagera kuwa ni pamoja na ni pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodailiwa chuoni, upatikanaji wa ajira wakati wa ujenzi hasa kwa wenyeji wenye sifa, huduma za kupangisha nyumba kwa wanafunzi na wafanyakazi wa chuo pamoja na wanafunzi wa shule za misingi kupata fursa ya kutembelea na kujifunza ili kuvutiwa na masomo ya teknolojia na biashara.
Naye, Dr. Edmund Mabhuye ambaye pia ni miongoni mwa mtaalamu wa mradi wa HEET kitengo cha Mazingira kutoka chuo kikuu cha UDSM amesema kuwa chuo hicho kitatoa kozi mbalimbali na kwa kuanza cha UDSM tawi la Kagera kitatoa kozi ya utalii, biashara pamoja na kozi ya ukalimu.
0 Comments