NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amefanya mkutano wa hadhara Katika kijiji cha Manushi Ndoo, Kata ya Kibosho Magharibi.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa Chama ngazi ya wilaya akiwemo Katibu wa CCM wilaya ya Moshi Vijijini Ramadhani Mahanyu na Katibu wa wazazi wilaya Andrew Mwandu.
Mbunge Ndakidemi na Diwani wa Kata ya Kibosho Magharivi, Prosper Massawe waliwasilisha ripoti ya kina ya miradi iliyotekelezwa kwenye kata kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita yenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 521.
Katika mkutano huo, wananchi waliwakilisha kero ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara zilizopo kwenye mtandao wa TARURA na zile za ndani.
Wananchi pia walieleza kero kubwa ya kukosekana kwa huduma ya maji ya mifereji kumwagilia mazao yao ya kahawa na migomba na kukosekana kwa nishati ya umeme kwenye baadhi ya maeneo.
Wananchi wamedai kuwa kukosekana kwa maji ya kumwagilia kumesababisha kuchelewesha maendeleo katika eneo la vijiji vya Manushi.
Kero ingine iliyowasilishwa ilikuwa ni changamoto ya gari la wagonjwa katika kituo cha afya Umbwe.
Katika mkutano huo, vijana walisimama na kulalamikia mikopo inayotolewa na halmashauri na kudai kuwa vijana na watu wenye ulemavu hawajapata mikopo hiyo na wizi wa mifugo uliokithiri katika vijiji vya Manushi.
Wakijibu hoja na kero za wananchi, Mbunge walisema ni jukumu lake na viongozi wenzake kutafuta majibu ya kero zao na kuzipeleka sehemu husika.
Kuhusu kero ya barabara, Diwani na Mbunge walisema, kuna barabara zilizoko kwenye mtandao wa TARURA ambazo zimetengewa fedha na zitajengwa kwa kiwango cha changarawe.
Walisema, barabara ya Weruweru Sekondari - Manushi - Kombo imeombewa fedha za ukarabati kwa kiwango cha changarawe kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Akiwajibu wananchi kuhusiana na hoja ya maji ya kumwagilia kahawa na migomba, mbunge alisema ameshawasilisha ombi wizara ya kilimo la kuomba mfereji wa Makeresho ufanyiwe ukarabati mkubwa ili wananchi wa vijiji vya Umbwe na Manushi wafikishiwe maji ya uhakika ya kumwagilia.
Mbunge aliwaambia wananchi kuwa kupitia mfuko wa jimbo, kata ya Kibosho Magharibi itapatiwa mifuko 200 ya saruji na shilingi milioni moja ambazo zitanunua mchanga wa kukarabati mifereji ya kimkakati.
Ndakidemi amewaambia wananchi wenye kero ya nishati ya umeme wajiandikishe ili yeye na Diwani wazipeleke TANESCO.
Mbunge huyo akizungumzia kuhusu changamoto ya ukosefu wa gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Umbwe, alisema kuwa suala hilo alishaliwasilisha kwenye wizara husika na serikali iliahidi kuwa italifanyia kazi.
Kuhusiana na mikopo, mbunge alishauri vijana washirikiane na afisa maendeleo ya jamii wa kata ili asaidie vikundi vyote vya kata (vijana, akina mama na walemavu) vipate mikopo.
Ili kukabiliana na changamoto ya wizi, mbunge alishauri wananchi wajipange na kujenga kituo cha polisi kwani kata yote ya Kibosho Mashariki yenye vijiji kumi hakuna kituo cha polisi.
Alitoa wito kwa wananchi kumpa ushirikiano inspector aliyepangwa kata ya Kibosho Magharibi kukabiliana na vitendo vya kihalifu.
Akiongea katika mkutano huo, Katibu wa CCM wilaya Ramadhani Mahanyu amewaomba wananchi wote kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, mbunge Ndakidemi na Diwani Prosper Massawe katika uongozi wao ili kuwapa moyo wa kuwatumikia Wananchi.
Mwisho..










0 Comments