Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda akiwaasa Wanafunzi kuwa na maadili mema.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mikiga Tedrick Komba akitoa taarifa ya shule hiyo.
Kushoto ni Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari Mikiga na meneja wa Shule hiyo ambao ni mapacha ,kulia ni mkuu wa Shule hiyo Tedrick Komba.
Wanafunzi wa kidato cha kwanza wakikaribishwa
xxxxxxxxxxxxxxxxx
Na Amon Mtega, Mbinga
MBUNGE wa Jimbo la Mbinga mjini Mkoani Ruvuma Jonas Mbunda amewataka Wanafunzi kuachana na tabia ya kujiingiza kwenye makundi maovu jambo ambalo huwapelekea baadhi ya Wanafunzi hao kutokufanya vyema kwenye masomo yao.
Mbunda ameutoa wito huo wakati akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mikiga iliyopo Mbinga inayomilikiwa na watu binafsi ,wakati wa hafla fupi ya kuwakaribisha Wanafunzi 72 wa mwaka wa kwanza katika hafla hiyo iliyoudhuliwa na watu mbalimbali wakiwemo wazazi wa wanafunzi hao.
Mbunge huyo amesema kuwa baadhi ya Wanafunzi wamekuwa wakifanya vibaya kwenye masomo yao ni kutokana na makundi maovu wanayokuwa wameambatana nayo,hivyo ni vema kila mwanafunzi anapokuwa na rafiki yake amchunguze kwa kina tabia za rafiki huyo kama ni njema au siyo njema ili asiweze kujiingiza kwenye mambo maovu.
Mbunda licha ya kuwahusia Wanafunzi hao lakini ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa kusimamia maadili kwa Wanafunzi hao pamoja na hatimaye kuwa na ufaulu uliokuwa mzuri na kuifanya shule hiyo kuwa kati ya shule zinafanya vizuri kiwilaya na kimkoa.
Aidha Mbunge huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo amesimamia zoezi la kuwagawia zawadi zilizotolewa na wamiliki wa shule hiyo kwa baadhi ya Wanafunzi wa kidato cha pili ambapo sasa wapo kidato cha tatu kwa kufanya vizuri mitihani yao ya kidato cha pili pamoja na walimu wao .
Nje ya zawadi zilizotolewa na shule hiyo Mbunge huyo ametoa mipira miwili kwa wasichana na wavulana pamoja na jezi kwa makundi yote mawili ili kuwafanya Wanafunzi hao katika kipindi cha michezo pasiwepo na kundi ambalo halishiriki michezo.
Kwa upande wake mkuu wa Shule hiyo Tedrick Komba amesema kuwa shule hiyo kwa miaka mitano mfululizo imekuwa ikiongeza ufaulu ambapo wahitimu wa kidato cha nne katika msimu uliyopita hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la nne ni daraja la kwanza hadi la tatu.
Mkuu huyo amesema kuwa sababu kubwa ya kuongeza ufaulu kwa Wanafunzi ni uwepo wa mazingira mazuri ya kujisomea pamoja na walimu kusimamia maadili na kukazana kuwafundisha.
Naye mkurugenzi wa Shule hiyo Michael Ndunguru na meneja wake Lucas Ndunguru (Fupi) ambao ni pacha wamesema kuwa shule hiyo ina miaka kumi tangu waianzishe ,huku lengo ilikuwa ni kutoa fursa kwa mwanafunzi pamoja na mzazi kuchagua shule ya kusoma na kuondoa visingizio vya kusema shule zipo chache.
Kwa upande wake mmoja wa wanafunzi Lilian Mbunda amesema kuwa licha ya shule hiyo kuwa na mchanganyiko wa wanafunzi wa kike na wakiume hakujawa na shida yeyote kwani kila mwanafunzi anazingatia nidhamu na maelekezo wanayopatiwa na walimu ,na kuwa kumekuwepo na mabweni ya jisia zote jambo ambalo huwafanya waweze kujisomea bila bugudha yeyote.
Hata hivyo mwanafunzi huyo alimshukuru Mbunge huyo kwa kutoa vifaa vya michezo mipira na jezi huku akisema vitawasaidia kwenye somo la michezo na pindi wanapofanya michezo ya kushindana na timu mbalimbali za kutoka kwenye shule nyingine.
0 Comments