Header Ads Widget

CHUNYA KUZALISHA 265,635 ZA MAZAO YA CHAKULA NA BIASHARA

Na Matukio Daima Media App

Chunya

KUELEKEA msimu wa kilimo wa mwaka 2026, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya inakusudia kuzalisha jumla ya tani 265,635 za mazao ya chakula na biashara yatakayolimwa kwenye eneo la hekta 83,420.

Akizungumza na Matukio daima Afisa Kilimo na Mkuu wa Sehemu ya Kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Paul Lugodisha amesema kuwa Halmashauri hiyo hufanya makisio ya uzalishaji kila mwaka kulingana na mwenendo wa uzalishaji wa mazao katika wilaya hiyo.



Amesema kuwa kwa upande wa mazao ya biashara, lengo ni kulima hekta 46,327 na kuzalisha tani 60,750.


“Moja ya kazi zetu muhimu ni kufanya makisio ya uzalishaji kulingana na mwenendo wa kilimo wilayani Chunya. Mahitaji yetu ni kulima mazao ya chakula na biashara ili kuhakikisha uzalishaji unaongezeka na mkulima ananufaika,” amesema Lugodisha.


Ameeleza kuwa ili kufikia malengo hayo, halmashauri imejiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo kuhuisha taarifa za wakulima kabla ya msimu wa kilimo, kuwasajili wakulima wapya na kuhakikisha wananufaika na mpango wa Serikali wa utoaji wa pembejeo za ruzuku.


“Halmashauri ipo katikati ya wakulima na mawakala wa pembejeo ili kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati na zinauzwa kwa bei elekezi ya Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea. Pia tunatoa elimu kuhusu kuzingatia kanuni bora za kilimo kuanzia maandalizi ya shamba, upandaji hadi palizi,” amesema.


Aidha, amesema kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi ya kilimo na kuzingatia kalenda ya kilimo ya wilaya. Ameongeza kuwa elimu ya matumizi ya mbegu bora inaendelea kutolewa kwa kuzingatia aina za mbegu zinazofaa kwa ukanda wa Chunya.


Kuhusu mashamba darasa, Lugodisha amesema kuwa kutokana na idadi ndogo ya maafisa ugani, halmashauri imekuwa ikiwakusanya wakulima kwa pamoja ili kuwapatia elimu kupitia mashamba darasa, ambapo wakulima waliopata elimu huwasambazia wenzao maarifa hayo.


Kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2026, amesema mahitaji ya pembejeo yanajumuisha tani 19,264 za mbolea, lita 34,838 za viuatilifu vya miminika, kilo 12,250 za viuatilifu vya baisi na tani 351.71 za mbegu bora za aina mbalimbali.


Kwa upande wake, John Kangala, mkazi wa Kata ya Sangambi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, amesema kitengo cha kilimo kimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima kwa kuwapatia elimu ya matumizi sahihi ya mbegu bora na maandalizi ya mashamba.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI