Header Ads Widget

KANISA KATOLIKI LAISHTAKI CCM KORTINI

 

Picha ya Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Joseph R. Mlola

Moja ya jengo la Shule ya Sekondari Chumvi Uvinza inayodaiwa kujengwa na CCM kwenye eneo la mgogoro.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxx

NA MWANDISHI WETU, MATUKIO DAIMA APP, Kigoma

KANISA Katoliki Jimbo la Kigoma limekishtaki Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai ya kuchukua eneo lao la ardhi bila ridhaa yao.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa hivi karibuni katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Kanisa hilo  limewashtaki Bodi ya Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Halmashauri ya Uvinza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuchukua eneo lao bila ridhaa yao.

Maombi hayo yamewasilishwa chini ya hati ya dharura na yamepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Lameck Mlacha wa mahakama hiyo.

Kupitia Wakili wa kujitegemea wa mkoani Kigoma, Method R.G Kabuguzi waombaji katika shauri hilo wanadai mjibu maombi namba mbili Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Halmashauri ya Uvinza wamepanga kuchukua eneo lao kuwapa CCM bila ridhaa yao kwa ajili ya kujenga madarasa ya Shule ya Sekondari ya Chumvi.

Kanisa Katoliki wanaiomba Mahakama hiyo ikubali kutoa amri ya zuio la muda kwa wajibu maombi na mawakala wao au watu wengine kujenga au kuendeleza eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 39.6.

Inadaiwa eneo hilo linalobishaniwa lipo jirani na eneo lingine la mwombaji (Kanisa) lenye ekari 21.4 lenye hati namba 4231 na lipo Kijiji cha Nyambutwe, Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Kupitia maombi hayo, Kanisa Katoliki linaiomba Mahakama iamuru wadaiwa wasifanye kitu chochote katika eneo hilo hadi shauri la msingi litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Kanisa Katoliki katika maombi hayo limewasilisha hati tatu za viapo zilizoapwa na Padri Esperius Hamenyande, Christopher Mibanda na Emmanuel Kimpanti.

Padri Hamenyande ni Mweka hazina wa Jimbo Katoliki la Kigoma na Christopher Mibanda ni Katekista mstaafu huku Emmanuel Kimpanti akiwa ni Mzee maarufu Uvinza. 

Katika viapo vyao wanadai mwaka 1920 Kanisa Katoliki waliomba eneo hilo kwa kiongozi wa Jadi wakati huo wakapewa ekari 61 maeneo ya Nyambutwe kwa ajili ya kujenga kanisa, shule, nyumba za watumishi, kituo cha afya na kuacha eneo lingine kwa ajili ya makaburi.

Wanadai mwaka 1934 ekari 21.4 zilipimwa na kupewa hati namba 4231, na eneo ambalo halikupimwa ekari 39.6 liliendelea kubakia chini ya kanisa hilo.

Mwaka 2020 CCM waliomba eneo hilo kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Chumvi lakini walikataliwa.

Inadaiwa Januari 4 mwaka 2021 Kanisa Katoliki liliandika barua kwa Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM wakitaka shule hiyo ihamishwe kutoka kwenye ardhi ya mgogoro lakini hilo halikufanyika.

Inadaiwa Julai mwaka 2022 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia barua yenye kumbukumbu namba CBA 166/171/01/57 alitoa maelekezo kwa Kanisa na Katibu Mkuu wa CCM akihimiza chama hicho kuhamisha miundombinu yao kwenye eneo lenye hati miliki ya Kanisa.

"Alielekeza Halmashauri ya Uvinza iandae mpango wa matumizi ya ardhi kwenye eneo ambalo halijapimwa na  ligawiwe kwa watu wengine.

"Waziri alielekeza eneo la makaburi lisitumike kwa maziko, maelekezo hayo yalichochea mgogoro,"alidai Padri Hamenyande katika kiapo chake.

Waombaji wanadai hawakukubaliana na uamuzi huo na wanaona hawakutendewa haki, wanaomba Mahakama ikubali maombi yao .

Mahakama imepanga shauri hilo litajwe Februari 15 mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS