Header Ads Widget

UTUNZAJI WA RASILIMALI ZA MAJI BADO NI CHANGAMOTO

 


Na Fatma Ally Matukio Daima APP Dar es Salaam


Licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maji Imeelezwa kuwa usimamizi bora wa rasilimali za maji ndio changamoto inayopelekea upungufu wa upatikanaji wa huduma za maji kwa wananchi.


Kauli hiyo, imetolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa la Taifa la wadau wa Sekta ya Mtambuka katika Usimamizi na Uendeshaji Rasilimali za Maji, Mhandisi Mbogo Futakamba alipokuwa katika mkutano wa wadau hao wakati wakitengeneza vikundi kazi vya wataalamu vitakavyotoa ripoti ya utendaji mwisho wa mwaka ili kuongeza ufanisi katika kutatua changamoto sekta ya maji.



Aidha amesema kupitia vikundi hivyo, watatengeneza mikakati ya kuwezesha upatikanaji wa fedha na usimamizi bora wa rasilimali za maji nchini ili ziwe na tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.


"Usimamizi wa rasilimali za maji hapa nchini bado ni changamoto, hadi sasa bado tunaimba wimbo wa utunzaji wa vyanzo vya maji lakini bado vinaendelea kuharibiwa matokeo yake sasa ni kukauka na jamii husika kukosa huduma ya maji hivyo niiombe jamii na wadau wa sekta ya maji kulinda vyanzo vyetu vya maji" amesema Mwenyekiti Futakamba.


Hata hivyo, ameziomba Sekta binafsi kuwekeza zaidi kwenye sekta ya rasilimali za maji ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi na kuondoa changamoto za baadhi ya maeneo kukosa maji kutokana na mabadiliko ya Tabianchi.


Aidha, amevitaka vikundi vitakavyoundwa kufanya uchaguzi kwa kuzingatia uwazi ili kupata viongozi watakaosimamia vyema rasilimali za maji hapa nchini kwa faida ya taifa na jamii husika.



Naye, Mratibu wa Mradi  wa Global Water Leadership, Asha Masoka wakati akitoa taarifa kwenye mkutano huo amesema kuwa kupitia makundi hayo matatu yaliyoundwa yataenda kuongeza uwekezaji, ubunifu, uvumbuzi na usimamizi wenye weledi katika sekta ya rasilimali za maji hapa nchini.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji,  George Lugomela amesema lengo la jukwaa hilo ni kuhakikisha uwepo wa ongezeko la ushiriki wa wadau wa sekta ya maji ikiwemo sekta binafsi katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji. 



Aidha amesema jukwaa hilo lipo kisheria na maoni yanayotolewa yanapelekwa kwenye bodi ya Taifa ya maji hivyo ni sehemu ambayo wadau wa sekta zote wanaweza kutoa maoni, mawazo, utaalamu na ujuzi wao katika kuhakikisha kuwa huduma ya maji inapatikana kulingana na mahitaji ya jamii.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI