Header Ads Widget

TANESCO YAJA NA MATUMANI MAPYA KWA WATANZANIA

 



Na Fatma Ally Matukio Daima APP Dar es Salaam


Shirika la Umeme Tanzania TANESCO limesema limefanikiwa kupunguza makali ya upungufu wa umeme kutoka wastani wa kati ya megawati 200 hadi 250 wiki iliyopita hadi kufikia wastani wa kati ya megawati 100 hadi 150 wiki hii.


 Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu TANESCO Maharage Chande amesema  tayari wameshakamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kinyerezi namba II na umeshaanza kuzalisha megawati 45 za umeme  ambazo zinaingia kwenye Gridi ya Taifa kuanzia tarehe 24 Novemba 2022. 


Amesema kuwa,  wamekamilisha ufungaji wa mitambo miwili iliyopo katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I na inaingiza megawati 90 za umeme kwenye Gridi ya Taifa.


Aidha, amesema kuwa licha ya kuongeza megawati hizo lakini bado wanaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa tatizo la uhaba wa umeme linaisha ambapo kwa sasa majaribio ya mtambo mmoja uliopo katika kituo cha Ubungo namba III yanaendelea na utazalisha megawati 20 za umeme kwenye Gridi ya Taifa kabla ya mwisho wa mwezi Disemba 2022.


Ameongeza kuwa, wanategemea mtambo mmoja uliopo katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I utaanza kuzalisha megawati 45 za umeme kwenye Gridi ya Taifa ifikapo Februari 2023. 



Aidha amesema wamekamilisha pia matengenezo ya mitambo miwili iliyopo katika kituo cha Ubungo namba III na imeshaanza kuzalisha kati ya megawati 35 na 40 za umeme kwenye Gridi ya Taifa kuanzia tarehe 25 Novemba 2022.


"Tayari tumeshakamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kidatu na umeshaanza kuzalisha megawati 50 za umeme kwenye Gridi ya Taifa kuanzia tarehe 30 Novemba 2022 pamoja na hizo megawati nyingine mtaona kuwa tumeongeza kiasi fulani cha umeme ambacho kitapunguza makali ya mgao wa umeme"amesema Mkurugenzi Chande. 


Amesema pamoja na mvua kuendelea kunyesha kwenye baadhi ya maeneo nchini, lakini bado hali ya kiwango cha maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme haijawa ya kuridhisha, hivyo wanaendelea na matengenezo ya umeme.


 "Kwa mfano; kituo cha New Pangani Falls (NPF) kwa sasa kinazalisha megawati 7 badala ya megawati 68, kituo cha Hale kinazalisha megawati 4 badala ya megawati 10.5, kituo cha Kidatu kinazalisha megawati 145 badala ya megawati 204 na bwawa la Nyumba ya Mungu linazalisha megawati 4 badala ya megawati 8, hali hii inalifanya Shirika kuendelea kutegemea zaidi uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia kuliko kwa kutumia maji"amesema Mkurugenzi Chande.


Amesema kuwa, Shirika litaendelea kutoa taarifa za hali ya umeme pamoja na kutoa ratiba za upungufu wa umeme kupitia tovuti ya www.tanesco.co.tz, kwa kuwatumia ujumbe mfupi wa maneno (SMS) na kwenye magroup ya whatsapp ya wateja wake nchini kote.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI