Na GIft Mongi, Moshi
Wananchi wa kijiji cha Miwaleni kilichopo katika kata ya Kahe Magharibi wameondokana na adha ya kuwapeleka watoto wao umbali mrefu Kwa ajili ya kuwapatia elimu ya chekechea baada ya shirika la FTK kujenga majengo ya vyumba vya madarasa kijijini hapo.
FTK ni shirika lisilokuwa la kiserikali ambalo lipo chini ya kiwanda cha TPC ambapo kupitia utaratibu wake wa ujirani mwema wamejenga vyumba hivyo Kwa lengo la kuwaondolea adha watoto kutembea umbali mrefu.
Akipokea majengo hayo mbunge wa jimbo la Vunjo Dr. Charles Kimei alishukuru FTK kupitia TPC kwa ufadhili huo na kuwa kunaenda kumaliza tatizo la watoto hao kutembea umbali mrefu.
"Niwashukuru sana TPC kwa hili mlilolifanya kwa kuhakikisha watoto wetu wanapata sehemu salama ya kusomea na huu ndio maana halisi ya dhana ya ujirani mwema"alisema
Hata hivyo mbali na kuwashukuru kwa mchango huo aliwakabidhi cheti cha shukrani kwa uongozi wa FTK kwa kutambua jitihada zao za kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu ndani ya jimbo la Vunjo.
"Nawaomba kwa gharama zote zile tukayatunze pamoja na miundombinu mingine ili iweze kudumu Kwa kipindi kirefu na malengo ya hawa wahisani yaweze kuleta maana"alisema
Katika hatua nyingine Dkt Kimei aliwahakikishia wananchi wa jimbo la Vunjo kwa jitihada mbalimbali anazozifanya za kuwatumikia hana shaka jimbo la Vunjo litazidi kupata maendeleo zaidi .
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa FTK, Uongozi wa Kampuni ya TPC, wajumbe wa bodi wakiongozwa na Cyril Mushi na Mtendaji mkuu wa kiwanda cha sukari T.P.C Jafari Ally.
0 Comments