Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAKALA wa barabara za mjini na vijijini (TARURA) mkoa Kigoma imesema kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 35.9 zilizotengwa na serikali kwa ajili ya miradi ya barabara na madaraja mkoani Kigoma kwa mwaka wa fedha 2022/2023 zitafanya barabara za mkoa huo kupitika wakati wote.
Sambamba na kuwezesha kupitika kwa barabara za mkoa huo wakati wote pia fedha hizo zitawezesha kufungua barabara za vijijini maeneo ya kiuchumi ya kilimo ambapo barabara zenye urefu wa kilometa 1275 na madaraja 199 yatahusika kwenye utekelezaji wa bajeti hiyo kwa mkoa Kigoma.
Meneja wa TARURA mkoa Kigoma,Injinia Godwin Mpinzile alisema hayo katika kikao cha bodi ya barabara ya mkoa akitoa taarifa ya hali ya utekelezaji wa miradi ya barabara inayosimamiwa na TARURA mkoani Kigoma.
Mpinzile alisema kuwa kutolewa kwa fedha hizo ni utekelezaji wa mpango wa serikali ya awamu ya sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassani kuhakikisha mkoa Kigoma unaimarisha barabara zake ili ziweze kutekeleza mpango wa serikali wa kuufanya mkoa huo kuwa wa kimkakati kiuchumi.
Alisema kuwa mkoa Kigoma una barabara zenye urefu wa kilometa 4814 ambapo barabara zenye urefu wa kilometa 2000 sawa na asilimia 41.55 zina hali mbaya hivyo fedha hizo zitaweza kuimarisha barabara hizo na kufungua barabara mpya.
Meneja huyo wa TARURA mkoa Kigoma alisema kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 7.2 kimetengenezwa kwa ajili ya bajeti ya kawaida huku fedha nyingine zikitoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo mfuko barabara shilingi bilioni 7.2, fedha za maendeleo kutokana na tozo za mafuta shilingi bilioni 15.1, mfuko wa jimbo kila wilaya shilingi bilioni tisa huku shilingi bilioni 4.6 ikiwa ni fedha za mradi maalum.
“Pamoja na fedha hizo kutumika kuimarisha barabara kwa kuunganisha na barabara kuu ili kusaidia shughuli za maendeleo na uchumi wa mkoa pia utekelezaji wa miradi hiyo utazingatia kufungua barabara za vijijini maeneo ya kiuchumi,”Alisema Meneja huyo wa TARURA Kigoma.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa mkoa Kigoma ameeleza kusikitishwa na hali ya wakandarasi wanaopewa miradi ya ujenzi wa barabara mkoani humo kufuatia baadhi ya barabara kuharibika kwa kipindi kifupi, baadhi ya barabara hazijaisha lakini wakandarasi hawapo maeneo ya ujenzi na hasa wakati huu wa mvua inafanya barabara kuharibika.
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa mkoa ameshangazwa na maeneo ya hifadhi za barabara kutokuwa na uangalizi ambapo wananchi wanafanya mambo wanayotaka ikiwemo kujenga, kulima au kujimilikisha maeneo ya hifadhi za barabara kana kwamba hakuna wasimamizi jambo ambalo linachangia migogoro mikubwa baadaye baina ya wananchi wasimamizi wa barabara hizo.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho akiwemo Mkuu wa wilaya Uvinza, Hanaf Msabaha alieleza kushangazwa kwake na baadhi ya makalavati yaliyojenga kwenye barabara ya Simbo hadi Kalya mengi yakionyesha kutoboka katikati hali inayoashiria viwango vya ujenzi vinavyofanywa na wakandarasi wanaopewa kazi hizo.
0 Comments