Na Gift Mongi,MATUKIO DAIMA APP,MOSHI
Vijana wa vyama vya upinzani wametakiwa kuacha kuwahadaa watanzania na kuwapotosha kwa maksudi kuhusu deni la taifa kwani bado taifa lina sifa za kukopesheka tofauti na inavyoaminishwa na baadhi ya vijana kupitia mitandao ya kijamii.
Hata hivyo imeelezwa kuwa deni hilo la taifa ni stahimilivu na kuwa fedha zilizokopwa zimeenda kufanya miradi mikubwa ya kimaendeleo na hivyo deni litajilipa lenyewe na hakuna atakayeamuriwa kulipa deni hilo.
Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi(UVCCM)wilaya ya Moshi Vijijini Yuvenail Shirima amesema kuwa kwa sasa baadhi ya vijana ambao sio waelewa wamekuwa wakidanganya umma kuhusu uhalisia wa deni lenyewe ulivyo badala ya kusema ukweli na kukubali juhudi zinazofanywa za kukuza uchumi.
"Utabaini miradi ambayo imechukuliwa mikopo inajiendesha yenyewe mfano reli ya kisasa ya SGR ina maana itajilipa hadi deni litakapokwisha lakini kwa miradi tuliyojenga kwa fedha za ndani hatutozi kama ilivyo kwadaraja la Tanzanite"amesema
Kwa mujibu wa Shirima ni kuwa hakuna mtu au taasisi yoyote ya fedha ambayo inaweza kukopesha wakati mkopaji ana hali mbaya ya kiuchumi hivyo kwa mantiki hiyo bado nchi yetu inakopesheka tofauti na inavyoaminishwa na vijana wachache ambao wanatafuta mitaji ya kisiasa.
"Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anazunguka huku na huko kutafuta fursa kadri zinavyopatikana mradi kuhakikisha anaijenga hii nchi ila wapo wasioona haya yote tena ni maksudi na uzuri mikopo ni ya unafuu na kulipwa kwa muda mrefu hakuna atakayeenda kutoa fedha zake mfukoni kulipa deni"amesema
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo ni kuwa hakuna mtanzania yoyote atakayekuja kufuatwa nyumbani kwa madai ya deni la taifa na kuwa miradi iliyoelekezewa fedha hizo itaenda kujiendesha yenyewe na kurejesha mikopo hiyo.
Hivi karibuni waziri wa fedha na mipango Dkt Mwigulu Nchemba akizungumza katika kituo mojawapo cha luninga nchini amesema deni la taifa bado ni stahimilivu na kuwa sio kama ambavyo imekuwa ikisemwa na baadhi ya wanasiasa.
Amesema ukubwa wa deni lenyewe umejumuisha pia mikopo ya watu binafsi kupitia kampuni zao hivyo inapojulishwa na mkopo wa taifa deni linaonekana kubwa jambo ambalo alisema bado watu wanatakiwa kupewa elimu ya kutosha.
Haya yote yanatokea kwa sasa ambapo katika mitandao ya kijamii na makundi zogozi kukiwa na mijadala mbalimbali kuhusiana na kuendelea kupaa kwa deni la taifa lakini pia na njia stahiki za kuchukua kama taifa.
0 Comments