Header Ads Widget

WANANCHI WA WILAYA YA MOSHI WALAZIMIKA KWENDA WILAYA YA ROMBO KUFUATA HUDUMA YA MAJI SAFI NA SALAMA.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI.


WAKAZI  wa Kata za Mwika Kaskazini, na Mwika kusini, zilizopo  Wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro wanalazimika kufuata huduma ya maji safi na salama Wilaya ya Rombo kutokana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kushindwa kutoa huduma katika kata hizo.


Hayo yamebainishwa na Diwani wa kata ya Mwika Kaskazini Samweli Shao wakati akichangia taarifa ya utoaji huduma ya maji ya Muwsa kipindi cha robo ya kwanza Jula- Septemba 2022 katika mkutano wa kawaida wa baraza la Madiwani uliofanyika jana.



Shao alisema kuwa, kutokana na kero hiyo wananchi wamelazimika kwenda wilayani Rombo kufuata huduma ya maji safi huku akiiomba Serikali kuingilia kati kutatua tatizo hilo na kudai kuwa endapo kero hiyo ikikosa ufumbuzi itakigharimu Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi Mkuu 2025 na ule wa Serikali za mitaa 2024.


"Katika kitu ambacho kinaenda kukigharimu chama cha Mapinduzi katika kata ya Mwika Kaskazini ni tatizo la maji hili limekuwa kero kubwa kwa wananchi kwani wamelazimika kwenda wilaya ya Rombo kufuata huduma ya maji safi na salama hivyo Serikali inapaswa kuingilia kati kupata ufumbuzi wake" alisema Shao.



Naye Diwani wa kata ya Njia panda, Loveness Mfinanga alisema kuwa, kata hiyo ya Njia panda inakabiliwa na shida kubwa ya maji na kuwataka Muwsa kubainisha wazi ni lini mradi wa maji Miwaleni - Njia panda utakamilika.


"Awali Muwsa walishawahi kutueleza katika baraza hili la Madiwani kuwa mradi wa maji Miwaleni - Njia panda unaogharimu Bilioni 2.378 ungekamilika mwezi Agosti mwaka huu ili kutatua changamoto ya maji kata ya Njia panda lakini haujakamilika sasa leo watueleze ni lini huu mradi utaenda kukamilika" alihoji Loveness.



Naye Diwani wa kata ya Mwika Kusini, Daniel Mhanza alisema kuwa kata hiyo inahudumiwa na Muwsa lakini vijiji vya Kiraeni na Kimangaro havina huduma ya maji ambapo wananchi wamekuwa wakiteseka katika upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.


Diwani huyo alisema kuwa, ipo haja kwa Muwsa kuongeza kasi ya utoaji huduma kwani wananchi wanashinda ya huduma ya maji safi na salama huku pia akilalamikia gharama za kuunganishiwa maji kwa wananchi kuwa kubwa ikilinganishwa na umbali lililo bomba kubwa.



Naye Diwani wa kata ya Mbokomu, Samweli Materu alilalamikia kitendo cha wananchi kutozwa bili kubwa huku mabomba yakiwa hayatoi maji.


Aidha Diwani huyo alisema kuwa, katika kata hiyo yapo mabomba ambayo yamelazwa tangu mwaka 2021 lakini mpaka sasa hayatoi maji na kuwataka Muwsa kusema ni lini watatoa huduma ya maji safi na salama katika kata hiyo ya Mbokomu.


Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi wa Usambazaji maji na Usafi wa Mazingira Muwsa, Mhandisi Innocent Lugodisha alisema kuwa, maeneo hayo kabla ya kukabidhiwa Muwsa yalikuwa katika hali mbaya ambapo mamlaka hiyo imeendelea kuboresha huduma.



Mhandisi Lugodisha alisema kuwa, sio kweli mamlaka hiyo imeshindwa kutoa huduma na wameendelea kuongeza mitandao mipya pamoja na kuboresha iliyopo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma yenye uhakika.


Kuhusu mradi wa maji Miwaleni - Njia panda ujenzi wake umeshafikia asilimia 95 na wanatarajia kukamilika kwake ifikapo Mwezi Disemba mwaka huu.

Mwisho.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI