Header Ads Widget

2.9b/ ZAKUSANYWA KUTOKA MALIASILI ZISIZOREJESHEKA, ZANZIBAR


Wizara ya Maji, Nishati na Madini (WMNM) Zanzibar, imekusanya jumla ya shilingi bilioni 2.97  katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ikiwa ni mauzo ya mchanga na vibali kutokana na utaratibu  mzuri wa usimamizi pamoja kuimarika kwa mfumo wa kielektroniki wa maombi ya vibali vya Maliasili  Zisizorejesheka (Madini Management System).

Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri, WMNM  Shabaan Ali Othman katika kikao cha utekelezaji wa programu za Wizara kwa kipindi cha Julai –Septemba, 2022 katika kikao cha pamoja na kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kilichofanyika jana katika ukumbi wa ZURA Maisara, Unguja.

Alisema usimamizi mzuri pamoja na kuimarika kwa mfumo wa kieletroniki wa maombi ya vibali vya Maliasili  Zisizorejesheka umesaidia udhibiti wa mchanga ambapo Sekta ya Madini imekusanya shilingi 2.97 bilioni sawa na asilimia 120 ya makadirio ya  kukusanyo 2.46 bilioni.

Pia alisema Idara ya Nishati na Madini imeimarisha kikosi cha doria kwa dhamira ya kudhibiti uchimbaji holela wa mchanga hivyo Idara hiyo imenunua gari tatu ambazo zitatumika katika doria kwa maeneo mbali mbali ya Unguja.

Alisema  kikosi cha doria pia kilipatiwa mafunzo ya ukaguzi wa vibali na leseni  pamoja na kuwapatiwa vifaa vya mawasiliano ili kurahisisha mawasiliano baina yao kwa ajili ya kuleta ufanisi katika kudhibiti maliasili hizo.

Aidha alisema Idara ya Nishati na Madini ilitumia shilingi milioni 100 kuwalipa fidia wananchi 23 ambao mazao yao yalithirika  kutokana na shughuli ya uchimbaji Maliasili Zisizorejesheka katika maeneo yao.

“Mheshimiwa Mwenyekiti Wizara ilipangiwa kukusanya  shilingi 2.46 bilioni kutoka katika vyanzo vya mapato yatokanayo na mauzo ya mchanga na vibali hadi kufikia 30 Septemba, 2022 Wizara imefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 2.97 bilioni sawa na asilimia 120 ya makadirio,” Alisema Othman.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Yahya Rashid Abdulla aliiagiza Wizara kukutana na Mkuu wa Wilaya  na vijana wanaouza mchanga eneo la TAVETA, ili kutafuta namna ya kudhibiti biashara hiyo katika eneo hilo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Nishati na Madini Mhandisi Said Haji Mdungi alisema  watalifanyia kazi  agizo hilo lilitolewa na  kamati hiyo, kwaajili ya kupata maoni mbali mbali ingawa Idara ya Nishati na Madini inatumia Sheria Na 3 ya mwaka  2015, Sheria ya Mazingira ya Zanzibar ambayo inamruhusu mtu kusafirisha Maliasili Zisizorejesheka na sio kuuza.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI