Header Ads Widget

WAKULIMA WATAKIWA KUFUATA USHAURI WA WATAALAMU KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI.

 


NA HAMIDA RAMADHAN, DODOMA

WAKULIMA  nchini Tanzania wameshauriwa kuwa makini hasa katika kipindi hiki cha kuandaa mashamba kwa kuhakikisha wanazingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo ikiwemo kuhakikisha wanapanda kwa mistari na kutumia mbolea ya samadi ili kuweza kurutubisha udongo ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.


Kauli hii inakuja wakati ambao, maeneo mbalimbali duniani yanaendelea kushuhudia athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.


Hayo yamesemwa na afisa kilimo wa Mkoa wa Dodoma Bernard Abraham pindi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.


Bwana Abraham amesema mabadiliko ya tabia nchi ni kumbukumbu za matukio ya hali ya hewa yaliyowekwa kwa muda mrefu ambayo sio chini ya miaka 30, katika hali hiyo ni eneo la Dodoma ndilo linalonekana.


Anasema Mkoa wa Dodoma wanaposema hali ya hewa  wanazungumzia mvua ambayo ipo katika vipengele vitatu ambavyo kipengele cha kwanza ni muda wa kuanza  kunyesha mvua  na kuisha mvua, cha pili  ni kiwango cha mvua na cha tatu ni mgawanyiko kwa maana ya eneo na muda yani imenyesha kwa siku ngapi katika maeneo gani. 


Asema Dodoma haiwezi kujitenga na dunia kwa kuwa  wote kilio chao  ni  suala zima la mabadiliko ya tabia nchi huku akitolea mfano jinsi Mkoa huo ulivyoathirika na tatizo hilo.


“Mfano mwaka jana msimu wa mvua 2021 /2022, mwezi Apili mvua  imenyesha mkoa mzima na asilimia kubwa ya mvua hiyo imenyesha  mwezi Februari na mwezi Januari,” anasema.


Amesema mvua ya uzalishaji katika sekta ya kilimo Mkoa wa Dodoma ilianza kunyesha mwezi Januari 15, mwaka huu wakati mabadiliko ya tabia nchi ya Mkoa huo imezoeleka kuanza kunyesha Novemba mwishoni na Disemba mwanzoni.


“Mwaka 2022 mvua imeanza kunyesha mwezi Januari katikati na ikaisha mwezi Machi  kwa wastani ni siku 45 ambazo ndizo zinatumika katika kupanda mbegu  au miche hadi zao kukua  hapa hazijaanza kuzaa lakini pia ikumbukwe maji yanahitajika ili zao liweze kuzaa,”amesema.


Na kuongeza, “mazao mengi mwaka huu yaliishia kwenye kukua hayakuweza kuzaa kwani mengi yalikosa maji ambapo  wilaya ya Dodoma Mjini zilinyesha jumla ya milimita 372 na hiyo mvua ilinyesha siku 37 tu na kati ya hizo zaidi ya nusu  ilinyesha mwezi Januari na mwezi Februari na wilaya hiyo iliyopata mvua nyingi ni Halmashauri ya Kondoa ilipata milimita 967.5 ilinyesha mwezi Januari.


Kwa upande  wake Meneja Habari na Mahusiano Martha Chassama kutoka Wakala wa Misitu (TFS)  amesema  kutokana na mabadiliko ya tabia nchi hali ya joto ya dunia imeongezeka na ni kwa sababu ya  kuwepo kwa gesi nyingi na kuharibiwa kwa tabaka la juu la uso wa dunia.


Anasema joto linapoongezeka kuna maeneo yana barafu kama vile kwenye milima, barafu huyeyuka.


Athari za kuyeyuka kwa barafu ni kuongezeka kwa kina cha maji kwenye bahari  kama inavyojulikana  kwenye bahari kuna visiwa, hivyo husababisha baadhi ya maeneo kumezwa na maji hayo.



NINI KIFANYIKE 


Amefafanua kuwa kurudishwa kwa uoto wa asili kuna ongeza kasi ya kupanda miti kwa jamii, serikali na hata mtu mmoja mmoja kupunguza shughuli za kibinadamu.


”Kila mwaka kuanzia mwezi wa tano hadi wa saba ni kipindi cha mavuno kwa wakulima mashambani lakini kwa mwaka huu ilikuwa ni tofauti  kwani bei za nafaka au vyakula katika masoko mbalimbali ya Dodoma yameonekana kuwa juu tofauti na matarajio ya Wananchi,”ameeleza.


Menas Muhumpa ni mkulima wa nafaka kutoka Wilaya ya Bahi Kijiji Cha Chifutuka na Mkondai alibainisha bei za nafaka kuwa juu imechangiwa na mvua kuwa chache hali iliyosababisha uzalishaji kuwa mdogo.


"Mategemeo yetu kama wakulima kwenye kila heka 1 ya shamba tupate gunia 10 lakini imekuwa tofauti kwa mwaka huu tumepata zaidi kwenye hiyo heka moja ni gunia 2 hadi 3 na hii yote inasababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi,”amesema.


Ameongeza kuwa, kuchoka kwa ardhi na kulima kwa mazoea bila kutumia mbegu bora, mbolea na dawa za kuua wadudu mashambani inasababisha kuvuna mazao machache.


Kwa Upande wake Shida Kisidi mkazi wa Mlowa barabarani amesema hali ya chakula imekuwa ni tatizo katika eneo lao sio tu bei kuwa juu bali nafaka hizo zilikuwa hadimu, hazipatikani na hata zikipatikana zinauzwa bei ya juu ambapo debe 1 la nataka lilikuwa linauzwa   shilingi 5,000 ambapo  bei ilipanda  kufikia debe 1 la nafaka kufikia shilingi 14,000 hadi 15,000.


"Niiombe serikali ilione hili na itoe bei elekezi kwa wakulima kwani anayeathirika zaidi ni sisi wananchi wa chini ambao hatujiwezi.  Pia msimu ujao itoe pembejeo za kilimo kwa wakati ili kuepukana na changamoto kama hizi," amesema kisidi.


Akiongea kwa niaba ya wakulima wenzake Janeth Leave ambae ni mkazi wa Kijiji cha Mkulabi Kata ya Mpunguzi na mkulima wa mazao ya Alizeti, mahindi, mtama, karanga na uhele alisema mwaka huu  ni mwaka wa njaa kwani hakuna mkulima hata mmoja aliyelima na kupata magunia angalau 50 tu.


"Mwaka jana, tofauti na mwaka huu, kwani mvua ilikuja kwa wakati wakulima tulilima kwa wakati na hata kilipofika kipindi cha mavuno kwa kweli tulipata mavuno mengi na ya kutosha. Ila mwaka huu, naona mabadiliko ya tabia nchi yameanza kuonekana kwani naweze kusema ile kauli ya jembe halimtupi mkulima ni tofauti. Ukweli ni kwamba, mwaka huu jembe limetutupa wakulima,"alisema Janeth.


Hata hivyo kutokana na hali hiyo,  Shirika la ActionAids  limewakutanisha vijana na wanawake wakulima kutoka mikoa yote ya Tanzania lengo likiwa ni kuona namna ya kukabilina na tatizo hilo. 


Mratibu wa vijana kutoka shirika hilo, Darif Fezal amesema wamekuwa wakifanya mikutano ya mara kwa mara ili kuwakutanisha kwa lengo la kujifunza dhana ya mabadiliko ya tabia nchi kwa hapa nchini Tanzania na namna ya kujiandaa na mabadiliko hayo.


Alisema kama inavyofahamika hivi karibuni yamefanyika majadiliano ya kidunia ya mabadiliko ya tabia nchi yaani COP 27 mkutano uliofanyika huko nchini Misri ambapo viongozi mbalimbali wa dunia na wanaharakati na wadau wa masuala ya mazingira wamekutana kujadili na kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo.


"Hivyo tumewakutanisha vijana na wanawake hawa wakulima mara kwa mara lengo ni kuzungumza, kujifunza na kuangalia kutokana na uzoefu wao na kuandaa neno litakalozungumzia hali ilivyo kwao na matarajio yao baada ya huo mkutano wa COP 27,"alisema.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI