NA HADIJA OMARY, LINDI
MKUU wa Mkoa wa Lindi Bi Zainab Telack amewataka Wakandarasi waliosaini mikataba ya kutengeneza Barabara Mkoani Lindi, kufanya kazi kwa weledi, uzalendo na kuhakikisha wanazikamilisha kwa muda uliopangwa.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Lindi Mkuu wa Wilaya hiyo Shaibu Ndemanga katika hafla ya utiaji saini wa mikataba 21 kati ya Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)Mkoa wa Lindi na wakandarasi 21 watakaotekeleza miradi ya barabara katika wilaya za Mkoa wa Lindi.
Ndemanga amesema ipo tabia ya baadhi ya wakandarasi kutengeneza barabara chini ya viwango na wengine kuchelewesha mradi kwa uzembe jambo ambalo limekuwa likitia doa kwenye sekta yao hivyo amewataka kukamilisha kazi walizopewa kama mikataba yao inavyoeleza.
Ndemanga alisema endapo kutakuwa na changamoto wafuate utaratibu wa kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo ili kushughulikiwa kabla Serikali haijaaza kuchukua hatua kali dhidi yao kutokana na ucheleweshwaji wa miradi hiyo
Aidha,Ndemanga alitumia nafasi hiyo kuwaelekeza TARURA Mkoani humo kuwasimamia wakandarasi hao kwa ukaribu zaidi ili wakamilishe miradi hiyo kwa wakati.
Kwa upande wa Meneja wa Tarura Mkoa wa lindi mhandisi Filbert Mpalasinge amesema mikataba hiyo iliyosainiwa ina thamani ya shilingi Bilion 9.6.
Mparasinge alisema TARURA Mkoa wa Lindi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imefanya manunuzi ya kupata Wakandarasi wa kutekeleza mikataba 48 yenye thamani ya shilingi 15,969,906,654.80; iliyosainiwa tarehe 25 Julai, 2022 ambapo Kazi zinaendelea kutekelezwa kwa hatua mbalimbali kwenye Wilaya zote.
Aidha mparasinge pia alieleza kuwa awamu ya pili, jumla ya Mikataba 22 imesainiwa jana Novemba 21 , 2022 ambapo Mikataba hiyo ina Thamani ya Shilingi 9,365,801,765.00.
Alisema kutia saini kwa awamu ya hiyo ya pili, kunakamilisha zoezi la manunuzi kwa asilimia 99. ambapo umebakia mkataba mmoja wa ujenzi wa daraja Wilaya ya Kilwa; ambayo upo hatua ya kukamilisha usanifu na baada ya usanifu, zabuni itatangazwa ili kumpata Mkandarasi atakae jenga daraja hilo.
"Jukumu kubwa tulilo nalo Wataalamu ni kuwasimamia Wakandarasi hawa kwa weledi, uadilifu na uzalendo ili kupata thamani ya fedha iliyokusudiwa. Tunawaomba Viongozi wetu wa Mkoa kushirikiana nasi katika kutekeleza kazi zetu ili tufikie malengo kwa pamoja"
Katika hatua nyingine Mparasinge alisema kuwa wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Lindi unasimamia Mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa kilometa 4,803.503. Kati ya hizo, urefu wa Kilometa 72.092 ni barabara za Lami; Kilometa 1,123.414 ni barabara za Changarawe na Kilometa 3,607.997 ni za udongo.
" Sehemu kubwa ya mtandao wa barabara za Mkoa wa Lindi ni barabara za udongo (Kilometa 3,607.997) sawa na asilimia 77.19 ya mtandao wote. Kutokana na hali hii ya barabara; ni wazi kuwa TARURA inalo jukumu kubwa la kuboresha mtandao wa barabara kutoka hali ya udongo kwenda kiwango cha Changarawe na Lami" alieleza Mparasinge .
Kwa upande wake Rais wa chama makandarasi wanawake Tanzania na Mkurugenzi wa Judex Contractors Ltd Maclesence Makala alisema pamoja na kwamba kazi zao zinategemea hali ya hewa katika wakati husika lakini wamejipanga kutekeleza miradi hiyo kwa weledi kwa wakati uliopanga
0 Comments