MHANDISI wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Brighton Kishoa amepewa adhabu ya kukatwa asilimia 15 ya mshahara wake baada ya kushindwa kusimamia mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi.
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ndiyo lililomchukulia hatua Mhandisi huyo kukatwa fedha hizo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Akitoa maazimio ya kikao hicho cha baraza la madiwani cha robo mwaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Musa Ndomba amesema kuwa mtumishi huyo alisababisha mradi huo kuwa na gharama kubwa.
Ndomba amesema kuwa ajenda ya mtumishi huyo iliyojadiliwa na baraza hilo na kubaini makosa ya kinidhamu ya kiutumishi yaliyofanywa na Mhandisi huyo.
"Moja ya changamoto kwenye ujenzi huo ambapo hakufuata utaratibu wa manunuzi (BOQ) ya ujenzi wa nyumba hiyo na kusababisha gharama za ujenzi huo kuwa kubwa,"amesema Ndomba.
Amesema baada ya changamoto hiyo kutokea ilibainika kuwa katika usimamizi wa miradi ilionekana kuna maeneo kafanya uzembe hivyo baraza la madiwani na kamati ya fedha ziliamua kumchukulia hatua za kinidhamu.
"Taratibu zote zimefuatwa kwa kamati za uchunguzi na kufanya kazi yake na zikapendekeza adhabu hiyo na hilo litakuwa fundisho kwa watumishi wengine kwa kutakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazowaongoza," amesema Ndomba.
0 Comments