Header Ads Widget

WAZAZI WATAKIWA KUWAPATIA MAHITAJI MUHIMU WATOTO WAO BADALA YA KUACHA WAJITAFUTIE WENYEWE.

 


WAZAZI Mkoani Pwani wametakiwa kuwapatia watoto wao mahitaji yao ya Msingi badala ya kuwaacha wajitafutie wenyewe.


Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Kaimu Kamishna wa Elimu Bahati Chikwindo wakati wa mahafali ya 16 ya kidato cha nne Shule ya Sekondari ya kutwa ya Nyumbu.


Chikwindo alisema kuwa wazazi wana wajibu wa kuhakikisha watoto wao ambao ni wanafunzi wanapata mahitaji yao muhimu ili waweze kutimiza ndoto zao.


"Ili mtoto afikie ndoto zake lazima wazazi wachukue nafasi zao kwa kuwalea katika misingi ya malezi bora ili kuepuka watoto kuingia kwenye makundi mabaya,"alisema Chikwindo.


Alisema kuwa Wizara itasaidia shule hiyo kuhakikisha inakabili changamoto za shule hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la utawala.


"Tutasaidia pia upatikanaji wa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA ili wanafunzi waweze kupata elimu hiyo ambayo ni muhimu kwa kipindi hichi cha utandawazi,"alisema Chikwindo.


Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Juma Mrope alisema kuwa shule hiyo ndiyo shule inayoongoza kwenye Mkoa huo ambapo ina wanafunzi 2,136 huku wahitimu wa kidato cha nne walikuwa ni 460.


Akisoma risala ya wahitimu Ahmed Kikoto alisema kuwa wanahitaji viti na meza zaidi ya 300, wanahitaji maktaba, ukarabati wa sakafu na kuomba kujengewa ukumbi na wanawashukuru wadau mbalimbali kwa kuwapatia miradi mbalimbali ikiwemo wa Tehama na serikali kujenga shule shikizi ya Sofu ambapo imepunguziwa wanafunzi 75.


Mwisho.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI