NA TITUS MWOMBEKI, Matukio Daima App Kagera.
WANANCHI mkoani kagera wameipongeza serikali kwa ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi na Huduma VETA kilichojengwa kijiji Bulugo kata Nyakato halmashauri ya Bukoba vijijini mkoani Kagera.
Hayo yamesemwa na Haida Moses mkazi wa kijiji cha Bulugo halmashauri ya Bukoba vijijini katika mahojiano maalumu baada ya kufunguliwa kwa chuo hicho ambapo wamesema kuwa kutokana na ujenzi wa chuo hicho itasaidia kuwaondolea wazazi changamoto ya kuwalipia watoto nauli kubwa wakati wakienda mikoa ya jirani kupata elimu.
"Tunaipongeza serikali kwa kuweza kujenga chuo hiki katika mkoa wetu, kwani kitasaidia kutuondelea kero ya kuwapeleka watoto wetu mikoa ya jirani kama ambavyo tumekuwa tukifanya"
Ameongeza kuwa ujenzi wa chuo hiko ni chachu ya maendeleo mkoani hapo kwani wananchi wataweza kunufaika kupitia kufanya shughuli mbalimbali za kibiashara katika maeneo yanayozunguka chuo hicho suala litakalosaidia wananchi hao kujiingizia kipato.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kagera, Albert Chalamila wakati akitoa neno la utambulisho amesema kuwa chuo hicho kimejengwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya China na kimeghalimu shilingi Bil.22, huku akiwataka wananchi wa mkoa huo kuwapeleka watoto wao kwenye chuo hicho ili waweze kujipatia elimu na maarifa.
"Mkoa wetu umekuwa na jumla ya vyuo vya kati 38, hivyo nichukue nafasi hii kuwaomba wananchi mkoani kagera kuwaleta watoto wao katika vyuo hivi na vile vinavyoendelea vinavyoendelea kujengwa mkoani humo ili waweze kujipatia elimu na pamoja na maarifa yatakayowasaidia kujikwamua kimaisha"
Aidha amewataka wananchi mkoani huo kuchapa kazi kwa nguvu zao zote na kuachana visingizio mbalimbali ambavyo wamekuwa wakivitoa kuwa ni chanzo cha umasikini mkoani hapo.
Naye balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema kuwa Tanzania na China ni nchi zenye urafiki wa muda ndefu na wamekuwa wakishirikiana na katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo sekta ya elimu huku akisema kuwa ujenzi wa chuo hicho utawasaidia vijana kupata mafunzo ya vitendo pamoja na kukuza vipaji kwa vijana.
Kwa upande wake, waziri wa elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Adroph Mkenda amewashukuru wananchi wa mkoa Kagera hususani wa kijiji cha Bulugo kwa kutoa ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho huku akisema kuwa chuo hicho kitaweza kudahili wanafunzi zaidi ya 1000 kwa kozi za muda mfupi na 400 wanafuzi kwa kozi za muda mrefu.
Naye rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Samia Suruhu Hassan wakati akiwahutubia wananchi wa mkoa wa Kagera baada ya kushuhudia kukamilika na makabidhiano ya chuo hicho ameishukuru serikali ya Jamhuri ya China kwa kuchangia ujenzi wa chuo hicho huku akisema kuwa chuo hicho kimesheheni miundombinu ya kisasa huku akiwataka wananchi uwapeleka watoto wao chuoni hapo pamoja na kutumia miundombinu ya chuo hicho kwa uangalifu mkubwa.
"Nimezungikia chuo hiki katika Karakana zote nimejionea miundombinu ya chuo hiki, niya kisasa hivyo kazi ni kwetu kutunza majengo haya na miundombinu iliyopo"
Ameongeza kuwa atahakikisha kila wilaya hapa nchini inakuwa na chuo cha ufundi stadi kinachomilikiwa na serikali ili kuwasaidia watoto ambao wamekuwa wakishindwa kwenda kwenye vyuo binafsi kutokana na changamoto ya ada kubwa nao waweze kunufaika.
Sambamba na hilo amewaagiza viongozi katika mkoa wa Kagera kuhakikisha wanawatambua vijana watakaosomea chuoni hapo ili kupitia asilimia kumi zilizotengwa na halmashauri ziwezekusaidia kuwanunulia vifaa vitakavyotumiwa na vijana hao kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao chuoni hapo.
0 Comments