Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis
Hamza Khamis amewataka wananchi kuacha kuvamia na kuharibu vyanzo vya maji.
Pia amekemea tabia ya baadhi watu kufanya makazi katika maeneo
yasiyostahili yakiwemo kwenye vyanzo vya maji hali inayochangia uharibifu wa
mazingira.
Mhe. Khamis alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara na wananchi
wa eneo la Ubaruku Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati wa ziara ya Kamati ya
Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta.
Alionesha kutofurahishwa na uharibifu wa vyanzo hivyo mara baada ya
kutembelea eneo la Mto Ruaha na Mnazi katika kijiji cha Mwanavala vilivyopo
ndani ya hifadhi.
Naibu waziri huyo alionya tabia ya baadhi ya wananchi kufanya shughuli za
kibinadamu zikiwemo kuingiza mifugo na kufanya makazi katika maeneo yenye
vyanzo vya maji.
“Tumeshuhudia vyanzo vya maji vimeharibiwa sana, maji yale ndio yanayotusababishia sisi kuishi, maji yale ndio yanayosukuma umeme ukapatikana, maji yale ndio viumbe hai wanasurvive sasa tumeliona lile bonde kule hali ni mbaya, tukikaa kimya tutaelekea pabaya,” alitahadharisha.
Aidha, Mhe. Khamis alisema hajafurahishwa na tabia ya ukataji miti holela
inayofanyika katika baadhi ya maeneo hapa nchini hali inayosababisha uharibifu
wa mazingira.
Alisema endapo wananchi wataendelea na tabia ya ukataji miti mvua itakuwa
ni ndoto hali itakayosababisha ukame ambao ni chanzo cha ukosefu wa maji kwa
ajili ya mifugo na shughuli za kilimo.
“Ndugu zangu naomba niwaambie mazingira ndiyo kila kitu tusipoyatunza
mazingira hayatatutunza, cha msingi nataka nitoe wito Tanzania nzima watu
wapande miti, watunze vyanzo vya maji, watunze mazingira, watu waheshimu sheria
na taratibu zote zinazohusiana na masuala ya mazingira,” alisema.
Tayari Kamati hiyo imeshatembelea mikoa mbalimbali
na inaendelea na ziara yake kwenye mikoa mingine ya Iringa, Njombe na Ruvuma.
0 Comments