JESHI la Zimamoto na Uokoaji limesema kuwa limejipanga kuokoa mali za wawekezaji na linapotokea tishio au moto watafika ndani ya dakika tano.
Hayo yalisemwa na msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Nchini Puyo Nzalayamis kwenye maonyesho ya biashara na uwekezaji yanayofanyika Maili Moja Wilayani Kibaha alipotembelea kikosi cha jeshi hilo cha mkoa wa Pwani na baadhi ya mabanda.
Nzalayamis alisema kuwa sheria za kimataifa za Uokoaji zinasema kuwa kunapotokea moto au hatari yoyote lazima huduma ipatikane ndani ya dakika tano baada ya kupata taarifa.
"Tunazingatia sheria za kimataifa na za ndani za kuokoa kuwa ndani ya dakika tano kufika kwenye eneo la tukio kikubwa tushirikiane na kikubwa mtupe taarifa mapema kabla moto haujafikia hatua mbaya,"alisema Nzalayamis.
Alisema kuwa changamoto kubwa ni wananchi kuchelewa kutoa taarifa pale moto unapoanza ambapo wanaanza kuzima na wakiona wamezidiwa ndiyo wanatoa taarifa.
"Kifaa cha kwanza cha kuzima moto ni gari la Zimamoto ambapo kila mkoa kuna gari la Zimamoto na mpango kila mahali ikiwemo Wilayani kuwe na gari na jitihada ni kupata magari na vifaa ambapo magari 15 ya Utawala yamepatikana kikubwa ni mawasiliano pande mbili hatuwezi kujua wajibu mwananchi kutupigia na kutupa taarifa,"alisema Nzalayamis.
Akiwa kwenye banda la Tanesco mkoa wa Pwani alisema lazima kuwe na ushirikiano na itolewe elimu kuielimisha umma uielimishwe kwani wao wanawataalamu wa kujua kuwa chanzo cha moto kimetokana na nini kwani siyo kila moto unatokana na hitilafu ya umeme.
"Bajeti ya mwaka huu ni kupata magari mawili ya Zimamoto huku yale ya utawala yanaratibu ukaguzi ambapo sisi tuko kituoni muda wote kwa ajili ya kutoa huduma na hatuwezi kubuni kuwa kuna moto hivyo tunawashauri wananchi kutoa taarifa mapema,"alisema Nzalayamis.
Kwa upande wake mkuu wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Pwani Jenifa Shirima alisema kuwa wanaendelea kutoa elimu ya kujikinga na majanga na moto.
Shirima alisema kuwa hadi sasa wamefikia asilimia 70 ya shule pia kuwa na klabu kwa kushirikiana na skauti mwaka huu ambapo kwa mwaka huu limetokea janga moja tu la moto kwenye shule ya sekondari ya Mkuza Kibaha na baadhi ya shule zi wanafunzi wengi sana na ni vizuri kuwe na vingamua moto mfano usiku vikipiga kelele itasaidia kupambana na moto mapema.
0 Comments