MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Abdul Sharifu amesema kuwa chama kinahitaji viongozi madhubuti kuongoza nchi.
Sharifu aliyasema hayo Wilayani Bagamoyo alipokuwa akipokelewa na viongozi na wanachama wa CCM kumpokea baada ya kushinda nafasi hiyo.
Alisema kuwa chama hicho pekee ndiyo chenye uwezo wa kuongoza nchi hivyo lazima kiwe imara kwa kupata viongozi bora na wenye uwezo wa kuongoza.
"CCM ndiyo inayo uwezo wa kuongoza nchi hivyo lazima tupate viongozi bora wenye uwezo na tusipopata viongozi madhubuti na wenye uwezo,"alisema Sharifu.
Aidha alisema kuwa ili kufanikiwa kuwa na viongozi bora wanachama wanapaswa kuchagua viongozi bora na kuacha kuendekeza makundi ambayo hatapaswi kuendelezwa mara baada ya uchaguzi.
"Tuachanena makundi kwani uchaguzi umekwisha na nitachukua hatua kali kwa watakaoendeleza makundi ambayo hayapaswi kuwepo ili yasilete ugumu kwenye uchaguzi wa 2024 na 2025,"alisema Sharifu.
Aidha alisema kuwa Mpango kazi wake ni kuhakikisha kila kata inakuwa na ofisi kwa ajili ya shughuli za chama kwani baadhi ya kata hazina ofisi.
"Kila kata itoe Mpango kazi wake wa ujenzi wa ofisi kwani tunataka kila kata iwe na ofisi nzuri kwani sisi ni chama kikubwa hivyo haiwezekani kutokuwa na ofisi,"alisema Sharifu.
Kwa upande wake mwakilishi wa madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo Salum Mikugo alisema kuwa watafanya kazi na mwenyekiti wao ili chama kisonge mbele.
Mikugo alisema kuwa wao kama madiwani watahakikisha wanaleta maendeleo kwa wananchi kwa kushirikiana na chama.
0 Comments