Header Ads Widget

“HALMASHAURI DHIBITINI FEDHA ZA MAPATO YA NDANI”- RC RUKWA

 

Mamlaka za Serikali za mitaa katika mkoa wa Rukwa zimeagizwa kuongeza usimamizi wa makusanyo ya fedha za mapato ya ndani ikiwemo kudhibiti matumizi yake ili wananchi wanufaike na miradi ya maendeleo.


Akifungua kikao cha kwanza cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) mjini Sumbawanga (Jumatano Octoba 12, 2022) Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga alibainisha kuwa halmashauri pamoja na kufanya vema kwenye makusanyo lazima matumizi yake yadhibitiwe kwa mujibu wa sheria.


Sendiga alisema katika kipindi cha mwaka 2021/22 halmashauri za Rukwa zilikusanya shilingi Bilioni 9.3 sawa na asilimia 97 ya lengo  na kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 kipindi cha Julai hadi Septemba 2022 tayari halmashauri zote nne zimekusanya shilingi Bilioni 2.7 sawa na asilimia 26 ya lengo.


“Naendelea kuzielekeza halmashauri zote kuhakikisha wanakusanya zaidi kwani ninaamini halmashauri zetu zina mapato ya kutosha lakini tatizo nililoliona ni la usimamizi kwa baadhi ya watumishi pamoja na kudhibiti matumizi” alisisitiza Sendiga.


Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Sekretariati ya Mkoa Donatus Weginah alisema katika mwaka wa fedha 2021/2022 mkoa ulitengewa bajeti ya shilingi Bilioni 152 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo  sekta za elimu, utawala, maji, barabara, na afya ambapo hadi Juni mwaka 2022 ulikuwa umepokea shilingi Bilioni 120.


Wakichangia mada kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP) mkoa wa Rukwa Peter Mpinga alishauri Serikali kudhibiti uvuvi wa samaki wadogo kuingia kwenye masoko ya Sumbawanga ili kunusuru mazalia ya samaki kwenye Ziwa Rukwa.


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Kalolo Ntira alishauri wataalam wa mkoa na halmashauri kukaa na kubuni namna nzuri ya kuhakikisha soko la samaki wanaovuliwa Rukwa linahamishwa toka Tunduma kuja Sumbawanga ili halmashauri zipate mapato zaidi.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI