NA TITUS MWOMBEKI, Matukio Daima App KAGERA
CHAMA cha Watu Wenye Ulemavu wasioona (TLB)mkoani Kagera wameiomba serikali kutenga muda maalumu wa kukutana na watu wenye ulemavu ili kuwapatia elimu stahiki jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa ebola.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Chama cha Watu Wasioona (TLB) mkoani Kagera, Novath Mwesiga wakati akiongea na chombo hiki ambapo amesema kuwa wakati serikali ikiendelea kupambana na ugonjwa wa ebola serikali inaombwa kuwapatia semina maalumu watu wenye ulemavu itakayowajengea uelewa jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo.
“Tunaomba serikali iliangalie kundi hili maalumu inapotoa elimu kwa watu wengine jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa ebola basi na sisi ituandalie semina maalumu itakayotusaidia kupata uelewa mpana jinsi ya kujikinga na ugonjwa huu” alisema Mwesiga
Amewasihi watu wenye ulemavu kuwa wakati wakiwasubiri wataalamu wa afya kuwapatia semina hiyo wanatakiwa kuwa makini sana na kuepuka kushikana mikono ovyo na watu wengine kwani ugonjwa huo ni hatari na unasambaa kwa njia kuambukizwa.
Kwaupande wake Mganga Mkuu Manispaa ya Bukoba, Dkt. Peter Mkenda amesema kuwa serikali kwa kushirikiana na viongozi wa afya mkoani Kagera wanaendelea kutoa elimu kwa makundi yote likiwemo kundi la watu wenye ulemavu jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa ebola ili kuwanusuru wananchi hao dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo.
“Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kujikinga na ugonjwa huu wa ebola ikiwa ni pamoja na kupita maeneo mbalimbali tukitoa elimu kwa umma kwa njia ya matangazo ili wananchi waweze kuchukua taadhari dhidi ya ugonjwa huo, kwa upande wa watu wenye ulemavu tuandaa utaratibu maalumu wa kukutana nao hata kupitia vikao vyao ili kuweza kutoa elimu katika kundi hili”
Sambamba na hilo, ameongeza kuwa wanaandaa programu maalumu itakayosaidia kutoa elimu jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo hususani kwa watu wenye ulemavu huku akiwasihi wananchi wote wa mkoa wa Kagera kuendelea kuchukua taadhari zote zinatolewa na viongozi kupitia vyombo vya habari jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Amesisitiza kuwa, ugonjwa huu haujaingia nchini ila hizi zote ni njia za kujikinga na ungonjwa huu hatari kwasababu tayari umeikumba nchi ya jirani.
0 Comments