Na Fadhili Abdallah,Matukio DaimaAPP Kigoma
VIONGOZI wa madhehebu mbalimbali ya dini wamepewa jukumu la kutumia nafasi zao kwenye maeneo yao ya utoaji wa ibada kuifikia jamii kutoa elimu na uhamasishaji jamii kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.
Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma,Dk.Jesca Lebba alisema hayo akifungua semina ya siku mbili ya kujenga uelewa wa viongozi wa madhehebu ya dini kushiriki kwenye mpango mkakati wa serikali wa kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo ambao kwa sasa umeripotiwa nchini Uganda.
Dk.Lebba alisema kuwa kwa sasa serikali imechukua hatua kuhakikisha wadau mbalimbali wanashiriki kwenye mpango wa kuelimisha na kufikisha ujumbe kwa jamii kujikinga na ugonjwa huo.
Mganga huyo Mkuu wa mkoa Kigoma alisema kuwa wana imani madhehebu ya dini kwa kutumia viongozi wake wanayo nafasi kubwa ya kuifikia jamii na kufikisha ujumbe huo na kufanyiwa kazi kwa haraka.
Pamoja na hivyo alisema kuwa umechukua hatua mbalimbali kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo matangazo kwa njia ya mikutano, kutumia magari ya matangazo, vyombo vya habari na vipeperushi ili kuhakikisha kila eneo linafikiwa.
Sambamba na hilo alisema kuwa mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa vituo ambavyo vitatumika kupokea wagonjwa watakaobainika, kutenga magari yatakayotumika kubebea wagonjwa watakaobainika lakini pia wahudumu wa afya wamepatiwa mafunzo maalum ya kuhudumia wagonjwa watakaojitokeza hasa kwenye mipaka ya kuingia nchini na mkoani hapa.
Awali Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Interfaith Partnership, Asina Shenduli alisema kuwa mafunzo hayo ya siku mbili yanalenga kuwajenga viongozi hao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola, kuwa na uelewa wa ugonjwa huo sambamba na kuwahamasisha kutumia elimu waliyopata kuifikisha kwa waumini wao.
“viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana kwenye jamii kutokana na nafasi zao na kuaminika kwao ambako kunaweza kuwa nyenzo kubwa kutumia sauti zao kuifikia jamii na kufikisha ujumbe kuhusu mapambano ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola, Alisema Asina Shenduli Mkurugenzi wa Tanzania Interfaith Partnership.
Akizungumza katika mafunzo hayo Padre Castus Rwegoshora kutoka kanisa Katoliki mkoani Kigoma alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwao kama viongozi lakini pia kwa ajili ya kufikisha kwa wauimini wao ili kuweza kusadia waumini hao na viongozi wao kujikinga na janga na hilo.
Padre Rwegoshora alisema kuwa mkoa Kigoma na moja ya mikoa iliyo hatarini kukumbwa na ugonjwa wa Ebola kutokana nan a mwingiliano na nchi za ukanda wa maziwa makuu lakini pia watu wengi wanaosafiri kwenda mkoa Kagera ambao uko jirani na nchi ya Uganda ambako ugonjwa huo umeshawapata watu 54 na 19 wamefariki.
Mwisho.
0 Comments