NA HADIJA OMARY -MATUKIO DAIMA APP LINDI
MKUU Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga amesema Serikali Wilayani humo haitawavumilia wafanyabiashara wanaonunua korosho kwa kuwalangua wakulima maarufu kama kangomba
Ndemanga ameyasema hayo leo alipokuwa anazungumza na Matukio daima ofisini kwake wakati huu ambao wakulima wakiendelea kuokota korosho kwenye mashamba yao na kusubiri maghala ya vyama vya msingi kufunguliwa kwa ajili ya kuanza msimu wa uuzaji wa zao hilo kuanzia oktoba mosi 2022.
Ndemanga amesema kuwa serikali haitamuonea huruma mfanya biashara yeyete atakaebainika ananunua korosho kwa wakulima nje ya utaratibu wa Sarikali kwani kufanya hivyo ni kumnyonya mkulima.
Amesema korosho za msimu wa mwaka huu 2022/2023 zitauzwa katika mfumo wa stakabadhi gharani kama ilivyofanyika katika misimu iliyopita huko nyuma.
Hata hivyo Ndemanga pia amesema kwa msimu wa mwaka huu wamejipanga katika uhakiki wa ubora wa korosho na hivyo wakulima wanapaswa kuwa wakwanza kuhakiki ubora kabla ya kuzipeleka kwenye Amcos huku akiwataka pia viongozi kwenye vyama vya msingi kuwa makini katika upokeaji wa korosho.
Ndemanga ameomba wadau katika sekta hiyo kushirikiana kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kumkomboa mkulima wa korosho kwa kuwawezesha ili waendelee kulima zao hilo ambapo kwa msimu huu imewawezesha kwa namna mbalimbali ikiwemo kutoa pembejeo bure na kuimarisha ushirika.
Sambamba na hayo,amewahimiza wakulima wenye korosho kuanza kuhakiki akaunti zao za benki kabla minada haijaanza ili kuepuka usumbufu katika malipo ya fedha zao .
0 Comments