HAMIDA RAMADHANI, DODOMA
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa mzigo mkubwa katika mfuko wa bima ya Afya (NHIF)endapo hatua stahiki hazitachukuliwa katika kudhibiti magonjwa hayo,kuna hatari ya Mfuko huo kuelemewa na gharama za matibabu
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini hapa Waziri Ummy amesema kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanufaika wenye magonjwa yasiyoambukizwa na gharama zake, hali hiyo inaweza kuathiri uhai na uendelevu wa Mfuko.
Waziri Ummy alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha huduma za afya, bado kuna changamoto ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya wananchi wenye magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ambayo gharama zake ni kubwa.
“Kulingana na takwimu zilizopo,gharama za magonjwa yasiyo ya kuambukizwa zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 35.65 mwaka 2016/17 hadi shilingi bilioni 99.09 mwaka 2021/22,”
Na kuongeza kuwa“Gharama za kuhudumia wagonjwa wa saratani wanaopata tiba za mionzi na chemotherapia (chemotherapy services), kupitia Mfuko ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 22.5 mwaka 2021/22,”alisema.
Kwa upande wa huduma za matibabu ya figo kwa wanachama wanaopata huduma ya kuchuja damu (hemodialysis services), gharama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9.5 mwaka 2015/16 kufikia shilingi bilioni 35.44 mwaka 2021/22.
Pia idadi ya wagonjwa hawa wa figo imeongezeka kutoka 280 mwaka 2014/15 hadi kufikia 2,099 mwaka 2021/22.Gharama za matibabu ya moyo kwa wanachama wa Mfuko wanaopata matibabu ya upasuaji wa moyo (minimal and invasive cardiac procedures), ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 0.5 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 4.33 mwaka 2021/22.
Gharama za vipimo vya CT scan na MRI ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 5.43 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 10.87 mwaka 2021/22.
“Kwa muelekeo wa takwimu hizi, ni wazi kuwa kama hatutachukua hatua madhubuti kama nchi, kuna uwezekano wa Mfuko kwa siku za mbeleni kushindwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria,”alisema .
Hatua hizo zinaanzia katika ngazi ya mtu mmoja mmoja kwa kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia aina za vyakula tunavyokula, kuepuka uvutaji wa sigara na kufanya mazoezi .
“Pamoja na uwepo wa ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, sababu nyingine inayohatarisha uhai na uendelevu wa Mfuko huu ni vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma na wanachama wa Mfuko, vitendo hivi vinalenga kujipatia manufaa kinyume na utaratibu,”amesema
Mathalani katika mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya wataaluma 65 wamefikishwa katika mabaraza yao kutokana na kukiuka taratibu na miongozo ya taaluma za afya.
MAELEKEZO
Waziri Ummy ameelekeza NHIF kuimarisha mikakati yake ya kupambana na vitendo vya udanganyifu pamoja na kuimarisha matumizi ya Mifumo ya TEHAMA.
Vilevile, changamoto nyingine iliyopo ni uwepo wa kundi kubwa la wananchi wanaojiunga na NHIF kwa hiari ambao, takribani asilimia 99 ni wagonjwa.
Alisema Makundi haya ni kutoka katika Sekta rasmi binafsi pamoja na ile isiyo rasmi ambapo hadi kufikia mwezi Juni 2022, Mfuko unahudumia takribani wanufaika milioni 4.8 ikilinganishwa na wanufaika 691,173 waliokuwa wakihudumiwa mwaka 2001/02.
Hivyo uwepo wa takribani asilimia 99 ya wanachama waliojiunga kwa hiari ambao ni wagonjwa imekuwa ikiongeza gharama za matibabu zinazolipwa na Mfuko.
Aidha aliwatoa wasiwasi wadau wa NHIF wakiwemo wanachama, watoa huduma pamoja na watanzania wote kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa Mfuko huu unakuwa imara, endelevu na stahimilivu kwani kwa sasa, ni moja kati ya mfumo unaotumika katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa nchini.
Pamoja na kuwa na wanachama asilimia nane (8) tu ya Watanzania wote, vituo vingi vya kutolea huduma vinategemea mapato kutoka katika Mfuko kwa zaidi ya asilimia 70.
0 Comments