Na Amon Mtega, Namtumbo
MKUU wa wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Dkt.Julius Ningu ameipongeza kampuni ya Mantra Tanzania kwa kutoa miche 1100 ya miti kwa ajili ya kupanda kwenye chanzo cha maji cha mto Lumecha kata ya Msindo Wilayani humo ikiwa ni moja ya utekelezaji wa kauli mbiu ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira na kusababisha hewa ukaa inayozikumba Nchi nyingi Duniani.
Ningu ametoa pongezi hizo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lumecha wilayani humo walioshiriki katika zoezi hilo la upandaji wa miti kwenye chanzo cha maji cha mto huo.
Amesema kuwa kampuni ya Mantra Tanzania imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika wilaya ya Namtumbo hususani kwenye kuunga mkono kauli mbiu ya Rais Samia Suluhu Hassan juu ya utunzaji wa mazingira.
Aidha amewataka wananchi hao kujenga utamaduni wa kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kuacha kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji kwa madai kwamba upotevu wa vyanzo hivyo ni tishio kwa uhai wa binadamu.
Naye Diwani wa kata ya Msindo Remna Nchimbi amewataka wananchi wa kijiji cha Lumecha kutunza miti hiyo kwa faida ya vizazi vijavyo na kwa Serikali ambapo amedai kwamba zoezi hilo litakuwa mkombozi mkubwa katika kutatua changamoto ya ukosefu wa maji kijijini hapo.
Mhifadhi mazingira wa wilaya ya Namtumbo mkoani humo Kelvin Mnali amesema kuwa lengo kubwa la upandaji wa miti kwenye vyanzo mbalimbali vya maji ni kwa ajili ya kukabiliana na shughuli za kibinadamu zinazofanywa na baadhi ya wananchi katika vyanzo hivyo vya maji pamoja na changamoto ya tabia nchi.
Kwa upande wake Ofisa mahusiano wa kampuni ya Mantra Tanzania Khadija Pallangyo amesema kuwa wao kama wadau wa mazingira wanaunga mkono kauli mbiu ya Rais Samia Suluhu Hassan katika suala la upandaji wa miti kwenye vyanzo vya maji,uhifadhi na utunzaji wa misitu kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya hewa ukaa.
Pallangyo ameitaja aina ya miti iliyopandwa kwenye chanzo hicho kuwa ni Minyonyo ,Mingongoma pamoja na Mingwina ambayo yote inadaiwa ni rafiki wa maji kutokana na uasili wamiti hiyo na kuwa litakuwa zoezi endelevu katika utunzaji wa mazingira.
MWISHO
0 Comments