DIWANI wa Kata ya Korongoni Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Heavenlight Kiondo amemtaka aliyekuwa Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Juma Rahibu kuacha tabia ya kumpakazia uongo kuwa amekwenda kwake kumuomba msamaha huku akiwa ameshika jani ambalo ni maarufu kwa kabila la Wachaga la Sale.
Akizungumza na waandishi wa habari, Diwani huyo alisema kuwa, anashangazwa na kitendo cha Rahibu kutoka katika vyombo vya Habari na kudai kuwa amemwendea kwake huku akiwa ameshika jani la Sale na kumuomba msamaha na kudai kuwa sio kweli na Rahibu anafanya hivyo kujitafutia kiki.
"Hivi kati ya mimi na yeye ni nani wa kumuomba mwenzake msamaha yeye anajua aliyonifanyia amenitukania mpaka marehemu mama yake yeye ndio anapaswa kuja kwangu na sale kuniomba msamaha sio mimi kumfwata" alisema Heavenlight.
Diwani huyo aliendelea kudai kuwa, Rahibu ameamua kupika uongo huo ili kutafuta kura za huruma wakati huu ambao mchakato wa kumpata Mstahiki Meya mpya wa Manispaa ya Moshi ukiendelea.
Aidha alimtaka Rahibu kutambua kuwa aliyemuondoa madarakani ni Mungu hivyo kitendo cha kutoa maneno ya uongo ili kupata kura za huruma ni sawa na kuanzisha vita ya kupambana na Mungu na kumtaka kuacha tabia ya kuwazushia watu maneno ya uongo.
"Anayeweka mamlaka za Serikali ni Mungu na aliyemuondoa Rahibu madarakani ni yeye Mungu sasa nikupe ushauri wa bure mdogo wangu mrudie Mungu na ujute maovu yako uliyoyafanya umekuwa ukiwatolea maneno machafu Madiwani na viongozi wenzako" alisema Heavenlight.
Na kuongeza "mimi siwezi kuja kukuomba msamaha kamwe bali wewe ndio unapaswa kuja kuniomba msamaha na familia yangu tena ukiwa umeshika jani la Sale na hata usipofanya hivi mimi nimemwachia Mungu".
Heavenlight aliwataka wananchi wa kata ya Korongoni kuyapuuza maneno yaliyotolewa na Rahibu huku akiwaahidi kuendelea kuwapambania katika kuwaletea maendeleo.
Alipotafutwa Juma Rahibu kueleza ukweli wa jambo hilo aliendelea kudai kuwa Diwani huyo wa kata ya Korongoni akifika kwake kumuomba msamaha huku akiwa ameshika jani la Sale.
"Huyo ni muongo maana alikuja kweli kwangu akiwa ameshika jani la Sale na kuniomba msamaha nashangaa anaposema mimi nampakazia uongo" alisema Rahibu.
Mwisho
0 Comments