Adeladius Makwega-DODOMA.
Katika matini iliyotangulia tulimalizia kwa utani uliopo baina ya babu, bibi na wajukuu zao pia utani wa mama na kijana wake mdogo wa kiume mwenye umri kati ya mwaka 1-6 na nilieleza maana ya utani huo ambao haufanyi kwa mtoto wa umri huo wa kike.
Leo mwanakwetu ninasonga mbele zaidi kwa kuwatazama Wanyakyusa na utani baina ya mtoto wa kaka na dada ambao ni mabinamu. Ndani ya kabila hili kulitazama jambo hili kwa kina kumekuwa na mitazamo mbalimbali kutokana imani ya familia hiyo kwa dada au kaka.
Wapo ambao wanatazama katika dhana ya ushirikina hapo jambo la kuoana baina ya mtoto wa kaka na dada halifanyiki kuogopa ulozi huo kuhamia kwa kizazi kingine. Mathalani dada anaweza kuolewa na familia ambayo ni washirikina na wana imani za wachawi jambo hilo lilikuwa linapigwa kwa gharama zote.Hapo mtoto wa kaka hawezi kuoa mtoto wa dada yake kamwe kabisa.
Mtazamo wa pili ni ule unaamini kuwa pangine kaka au dada anao au kuolewa na familia ambayo wana miili iliyojengeka vizuri na afya njema pengine ndiyo hali ya familia ya baba na Mama waliowazaa Kaka na dada hawa, ili wasipoteze namna miili yao ilivyo basi hapo kuoana baina ya mtoto wa kaka na dada kunahimizwa mno.
Kwa dhana ya kizazi bora kisipotee mathalani Chifu wa Kinyakyusa alikuwa na muonekano fulani labda ni mtu mwenye mwili uliojengeka ambao unaonesha uhodari wa vita akimkamata adui anamdhibiti vizuri. Hapa koo nyingi za uchifu wa Wanyakyusa zilioana zenyewe kwa zenyewe.
Hapo inakuja hoja kuwa koo zote za Kichifu za Wanyakyusa zina udugu wa damu kwa hoja hii ya kuoleana baina ya binamu na binamu. Dhana ya udugu inakuwa kubwa zaidi kwa kuwa utani unakuwepo mkubwa na ndiyo maana hata chifu mmoja alipovamia Wanyakyusa wote walipambana na adui huyo mvamizi.
Kama ilivyo kwa makabila mengi ya Tanzania utani upo pia baina ya kabila na kabila lingine na utani huo mara nyingi chanzo chake kikubwa ni vita. Vita hivyo vilipiganwa kabla ya ujio wa Wazungu kuingia katika ukanda huu. Watani wakubwa kabisa wa Wanyakyusa na Wangoni, Wahehe na Wasangu. Ndiyo kusema kulikuwa na vita baina ya Wanyakyusa na Wahehe, Wanyakyusa na Wangoni na Wanakyusa na Wasangu.
Mngoni alifanya vita na Wanyakyusa kupitia Kaskazini Mashariki na Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi na Wasangu na Wahehe walifanya vita na Wanyakyusa kupitia Kaskazini Magharibi upande wa juu wa Wilaya ya Rungwe.
Wangoni hawa waliwachokoza Wanyakyusa walitokea huko Afrika ya Kusini na kuwachokozwa Wanyakyusa waliokuwa wametulia tuli katika maeneo yao huku makundi kadhaa ya Wangoni yakifanya uvamizi huo kila mara. Wangoni waliongia katika eneo hilo wakitokea Rhodesia, Malawi na Sumbawanga (Ufipa) na wakawa katika makundi makubwa mawili.
Ikiaminika kuwa uvamizi huo uliongozwa na bwana mkubwa mmoja aliyefahamika kama Mwandangala. Wangoni walipofika kati ya ukanda huu walipigwa vilivyo na kufurushwa huku wengine wakikamatwa. Mwandangala alikimbilia Mbeya alipofika huku alimsaidia mno Chifu wa Usangua Merere kumjengea ngome kubwa katika eneo linalofahamika kama Utengule umbali wa maili kama 10 uelekeo wa Zambia.
Kichwani kwa Mwandangala aliamini kuwa kama atashirikiana na na Chifu Merere na Wahehe basi hilo litamsaidia mno kuweza kupambana na Wanyakyusa.
Mwanakwetu nakukumbusha kuwa Mwandangala alikuwa Mngoni sasa anaunganisha nguvu na majirani wa Wanyakyusa ili apambane nao.
Majadiliano yalifanyika kwa kina hapo ndipo Wahehe na Wasangu wakaungana na Mwandangala ili kwenda kupambana na Wanyakyusa.
Kumbuka jambo moja kuwa Wasangu na Wahehe hawa walikuwa maadui tangu zamani wa Wanyakysa kubwa ni wivu ya ardhi yao, mifugo yao iliyonawili na kilimo chao kilichofanyika katika ardhi ya volkano ambayo mazao mengi yalimea huku maji yakipatikana sana.
Safari ya kwenda Rungwe vitani ilipangwa kwenda kuwamaliza kabisa Wanyakyusa.
Kabla yakwenda vitani huwa kunafanyika kikao cha vita ambacho kinapanga namna watakavyopigana na lengo la vita hivyo. Kikao hicho kilifanyika baina ya Chifu Merere, Mwandangala na viongozi wa Wahehe.
Ajenda ya msingi ni kuwamaliza kabisa na kutawala eneo hilo lakini kama hilo litashindikana walipanga kuwa wawakamate wanawake wa Kinyakyusa na ajenda ya tatu ilikuwa na kuteka mifugo yote ya Wanyakyusa na kuondoka nao.
Maswali la kujiuliza kwanini Chifu Merere, Mwandangala (Mngoni) na Viongozi wa Wahehe waliweka mezani ajenda za kuteka wanawake wa Kinyakyusa na kupora mifugo na kuondoka nayo?
Kwanini machifu hao wakubwa walizijadili ajenda hizo na kuwa mpango wa vita hivyo?
Je Wasangu, Wahehe na Wangoni hawakuwa na wanawake wazuri?
Mwanakwetu kwa leo naishia hapo.
Maswali hayo yote nitayajibu katika matini ijayo.
“Kulonda kukupa akapango kawaikulu Bhawakinyekyusa.”
Nitakumegea kipande cha siri ya wanawake wa Kinyakyusa.
Nakutakia siku njema.
makwadeladaius@gmail.com
0 Comments