Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amesema uwepo wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji ndiyo njia sahihi ya kuepuka migogoro ya ardhi ikiwemo ile ya wakulima na wafugaji kwa kuwa mpango huo unaanisha matumizi ya shughuli mbalimbali katika maeneo hayo.
Alisema, ndani ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kuna maeneo mbalimbali yameainishwa kama maeneo mahsusi kwa ajili ya shughuli za ufugaji na maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Ridhiwani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani alisema hayo leo katika mwendelezo wa ziara ya kusikiliza na kutolea ufafanuzi changamoto mbalimbali katika jimbo lake ikiwamo migogoro ya ardhi ambapo mpaka sasa amefanikiwa kutembelea Kata ya Miono, Vigwaza, Kibindu na Msoga.
‘‘Kila Mwenyekiti wa kijiji anapaswa kuwaelimisha wananchi wake juu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao umeainisha vitu vya msingi kama wapi wananchi watalima au kufuga, wapi wataishi, na shughuli nyingine za kimaendeleo zitafanyika lakini pia mpango huo umeainisha mipaka mbalimbali ndani ya kijiji ili wananchi wapate kufahamu mipaka na kuepukana na migogoro’’ alisema Ridhiwani.
Kauli hiyo ya Ridhiwani ameitoa baada ya wananchi wengi katika Jimbo la Chalinze kuwa na malalamiko mengi yanayohusu migogoro baina ya wakulima na wafugaji lakini pia migogoro ya mipaka baina ya kijiji na kijiji.
‘‘Kuuza kiholela maeneo yetu ndiko kunasababisha migogoro hii ya ardhi, eneo linaweza kuwa ni kwa ajili ya kilimo anauziwa mfugaji bila kufuata mpango wa matumizi bora ya ardhi hivyo tunaomba wananchi mnapotaka kuuza maeneo yenu muwasiliane na Serikali za vijiji ili kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi’’ alisema Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Bw. Musa Kichumu.
0 Comments