Na Adeladius Makwega-DODOMA.
Kwa hakika hali ya shule hii ya Tambaza sasa ilikuwa ya amani huku masomo yakiendelea kama kawaida. Kwa kuwa matini kadhaa zilizotangulia sikujibu maswali ya wasomaji wangu naomba leo nitumie wasaa huu kujibu swali moja.
Kwa hisani yako msomaji wa matini haya hii ngoja nilijibu swali la ndugu Fredrick Mwambene nayeye alikuwa mwanafunzi wa Tambaza kipindi hicho.
“Kaka Makwega unakumbuka yale mabasi ya wanafunzi aina ya TATA kwanini mradi ule wa mabasi ya wanafunzi haukuendelea?”
Kwa faida ya msomaji wangu ni kuwa huyu Fredy Mwambene tulikuwa tunakaa jirani naye Mbagala Sabasaba wakati huo, familia yao ina asili ya mkoa wa Songwe nachoweza kukumbuka zaidi hata siku ya kwanza kwenda kuanza kidato cha kwanza Tambaza tulikuwa pamoja.
Nakumbuka wakati tunasoma alikuwa bingwa na mpenzi wa somo la Kifaransa.
“Bonne apres midi”-Habari za mchana
“Comment vous appelez vous?”-Jina lako ni nani?
Hapo mwanakwetu najaribu tu kukumbuka lugha hiyo.
Ni kweli ndugu Mwambene na wasomaji wangu wengine kuwa mradi wa mabasi ya wanafunzi Dar es Salaam ulikuwa chini ya Umoja wa Vijana wa CCM mkoa huo, haukuweza kudumu kwa muda mrefu na kwa hakika haukufanya vizuri na ukafa.
Kuufahamu mradi huo naomba nirudi nyuma kidogo, suala la usafiri wa wanafunzi jijini Dar es Salaam lilisumbua mno wakati huo kwani awali Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) lilifanya kazi yake vizuri kuwasafirisha wanafunzi. Awali wanafunzi hao waliweza kuwa na tiketi za msimu, wazazi waliwalipia watoto wao na walipanda mabasi hayo kupitia milango ya mbele ya UDA.
Watu katika jiji la Dar es Salaam waliongezeka kwa kasi hapo ndipo zilipoibuka Daladala kwa wingi na kuweza kulimeza UDA huku likijikongoja.
Wafanyabiashara wa Daladala waliitafuta faida na kupakia wanafunzi wengi maana yake ni hasara hapo ndipo ugomvi na wanafunzi ulishika kasi na idadi ya wanafunzi sekondari ilikuwa maradufu
“Na kali kuliko zote ni upinzani konda na denti, wanaposhikana mashati denti anapoketi.”
Anasema Joseph Haule (Profesa Jay) katika wimbo wake wa Bongo Dar es Salaam ambao ulitoka wakati wa kipindi cha vita hivyo vya makondakta na wanafunzi ukionesha hali iivyokuwa.
Nakumbuka wakatii huo Augustino Mrema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alifika hadi Tambaza na katika kikao hicho na wanafunzi waliuliza maswali ya idadi ya wanafunzi wanaopaswa kupanda basi moja. Swali hilo alijibu RPC Typhone Maji. Swali la pili lilikuwa ni agizo la kuwekwa kwa siti ya wanafunzi katika mabasi madogo maarufu kama Hiace, hapa Waziri Mrema alimuagiza RPC Maji kulisimamia hilo.
Kwa hiyo dhana ya mabasi ya Wanafunzi ambayo lilikuwa ni wazo la UVCCM ya John Guninita walianza kutafuta fedha za kupata mabasi hayo.
Nakumbuka walimu wa madarasa walipatiwa kadi za kuchangia mabasi hayo na kuwapatia wanafunzi madarasani. Mimi nilipewa kadi hiyo na kumpatia Babu yangu ambaye alichangia Tsh 15000/=
Mradi ulianza kufanya kazi kwa hasara na baadaye kufa kwa kuwa ulikuwa mradi wa huduma na si faida.Pili magari ya awali yalikuwa machache , tatu mabasi hayo hayakuwa imara, nne mradi huo ulikuwa na mtaji mdogo na tano mahitaji yalikuwa makubwa kuliko huduma iliyotolewa.Sita UVCCM Dar es Salaam haikuwa na uzoefu wa kuendesha miradi ya huduma kama hiyo.
Binafsi ninasema kuwa UVCCM chini ya Uwenyekiti Taifa wa John Guninita ilijitahidi mno kwa kujaribu jambo hilo kwani ni heri ya kujaribu kuliko kutofanya jambo.
UVCCM ya sasa inaweza kuibuka upya na mradi kama huo kwani ni mradi kwa ustawi wa binadamu labda wanaweza kwenda mbali zaidi ya John Guninita na wenzake akina William Lukuvi.
Je kipi kitaendelea subiri matini ijayo.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments