Header Ads Widget

MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA X

 



Adeladius Makwega-DODOMA.


Katika matini iliyotangulia niliyoipa maneno yaliyokoza wino Mgogoro wa Azania na Tambaza ikiwa kama kitambulisho cha matini muendeleo zinazoelezea maisha katika shule ya Tambaza na maisha yaliyozunguka kipindi hicho. Nakumbuka nilimalizia na shule ya sekondari ya ST Antony ya Mbagala namna ilivyoanza.


Nilielezea namna shule hiyo ilivyoanza na nikahitimisha na msiba wa padri mwanzilishi wa shule hiyo Padri Fidelis ambaye kaburi lake lipo ndani ya eneo lililokuwa makao makuu ya Parokia ya Mbagala (Sasa ni Mbagala Spritual Centre).


Pia nilieleza siku ya msiba wa padri huyu muitaliano kutoka shirika la Wakapuchini, namna Balozi Paul Rupia na Peter Pinda walivyoshukuriwa kwa kuwasaidia shule hiyo mpaka kupata eneo la shule hii.


Maisha baada ya mechi baina ya Tambaza na Jitegemee kwa majuma mawili yalikuwa magumu mno kama nilivyoeleza huku harakati za gwaride la utambulisho, mara wengine mahakamani, wengine Segerea zilivyozizima.


Taswira iliyokuwepo kwa wanafunzi wengi wa Tambaza ilikuwa namna mabinti wa Jitegemee Sekondari walivyokuwa wakipita kuwatambua waliowafanyia vurugu katika gwaride la utambulisho.


“Tulichaniwa mashati yetu na wanafunzi wa Tambaza na tulirudi nyumbani kwa miguu kutoka taifa hadi Kiwalani.” 


Haya anasema Jane Mwaswala ambaye alikuwa miongoni mwa wasichana wa shule ya sekondari ya Jitegemee wakati wa tukio hilo.


Kwa desturi shuleni Tambaza palikuwa na wafanyabiashara wachache mno wa biashara ndogo ndogo kwani chakula kilikuwa kinatolewa shuleni bure nadhani msomaji wangu unamkumbuka Mpishi wetu Mama Rugangira.


“Mama Rungagira nifukuze basi.”


Huo ukiwa msemo maarufu mno pale tulipokuwa tukimfuata mama huyo kuomba chakula.


Jambo la kustajabisha mno palikuwepo na babu mmoja ambaye alikuwa akiuza karanga kila siku akizikaanga vizuri nyumbani kwake kuvifunga katika mfuko wake kati ya kilo mbili na tatu na ukitoa pesa ulipimiwa kulingana na pesa yako huku zikiwa za moto.


Babu huyu hakuwai kufanyiwa vurugu hata siku moja na hakuwai kuondolewa ndani ya shule hii kuuza karanga zake na ninakumbuka pia wanafunzi wa Tambaza pia hatukuwahi kujiuliza babu huyu mbona uongozi wa Tambaza ulimuacha afanye biashara yake na bila ya kukatazwa kuingia katika uzio wa shule hii? Mbona wafanyabiashara wengine hawakudiriki kufanya hivyo?


Babu huyu hakuwa na kiti bali alikaa chini ya mti wa Mkrisimasi na aliketi katika mizizi yake na kufungua karanga zake na kutupimia, jirani na madarasa ya kidato cha kwanza huku wanafunzi wakipiga soga naye iwe za mpira ya Simba na Yanga na hata habari juu ya mechi ya Tambaza na Jitegemee.


Babu huyu alitambulika kama mwanafunzi wa kudumu wa Tambaza.


Babu muuza karanga alikuwa maarufu mno na hata habari nyingi za wanafunzi wa Tambaza alikuwa nazo. Hata kama alipokuwa akirudi nyumbani kwake kama alijaliwa kuwa na wajukuu waliozaliwa na watoto wake au wale wajukuu wa hiari (wajukuu wa hiari) nina hakika walifaidi mno kwa simulizi tamu za vijana wa Dar es Salaam kutoka kila kona zote za mkoa huo waliokuwa wakisoma Tambaza.


Mara baada ya majuma mawili kuisha shuleni Tambaza hali illitulia na maisha yaliendelea kama kawaida huku wanafunzi wote tulipata wasaa wa kusimuliana namna mambo yalivyokuwa siku ya tukio la mechi hiyo.


Nakumbuka kuna wenzetu fulani walisimulia namna walivyotoka uwanja wa Taifa wakipita Keko Magorofani hadi Karume huku wakikimbia na wakafika Kigogo. Kwa kuwa hali haikuwa salama ilibidi waingie katika nyumba moja na kujificha angalau kusubiri hali itulie.


Walikaa hapo hadi saa tatu ya usiku baba wa nyumba hiyo alirudi na kukuta nyumba yao inawageni. Aliuliza jamani leo kulikoni? Alipokuwa anaingia kwa kuwa nyumba hii haikuwa na umeme wanafunzi hawa wa Tambaza hawakuweza kumuona vizuri kumbe baba huyu alikuwa askari wa Kituo cha Polisi cha Msimbazi akivalia sare zake na cheo chake cha Konstebo wa polisi.


Wanafunzi hawa wa Tambaza walitetemeka na kuomba msamaha wakitambua kuwa serikali kweli ina mkono mrefu, imeweza kuwatambua kuwa wamejificha katika nyumba hii. Kwa kuwa askari huyu alilifahamua tukio hilo aliwaomba kwanza wanafunzi hao wa Tambaza walale hapo hadi asubuhi ndipo waende makwao.


Wema huo wa Kostebo huyo wa polisi haukuwaingia akilini wanafunzi hao wakidhani kuwa ilikuwa ni janja ya nyani kula kunde mbichi ya kuwataka walale hapo alafu wakamatwe.


Wanafunzi hao muda huohuo waliaga na kuanza safari ya kwenda kwao kwa mguu hadi Kijtonyama.


Je kipi kitaendelea subiri matini ijayo.


Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI