WAJUMBE wa kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii wameshauri serikali kuongeza bajeti kwa chuo cha maendeleo ya jamii Rungemba wilayani Mufindi mkoa wa Iringa ili kusaidia kufanya maboresho makubwa ya majengo ya chuo hicho ambayo ni chakavu.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Stanslaus Nyongo alisema kuwa kamati yake imeridhishwa na kasi ya maendeleo katika chuo hicho .
Alisema kuwa, ukarabati na ujenzi wa miundombinu chuoni hapo yakiwemo mabweni na jengo la Utawala ni suala la lazima kwani itasaidia kuweka mazingira mazuri ya wananfunzi kufundisha na kujifunzia kwa kupata sehemu nzuri ya kulala na kushiriki masomo vizuri.
Aidha Nyongo alielekeza Wizara kuainisha maeneo yanayojitaji mchango wa Wabunge ili yatafutiwe ufumbuzi wa haraka ikiwemo kupatiwa fedha za maendeleo ili waweze kuboresha miundombinu Chuoni hapo.
"Pamoja na ripoti hii, nampongeza Mkuu wa Chuo ametueleza hali ya chuo na miradi inayotekelezwa lakini hali ni mbaya hatuwezi kufumba macho." alisema Nyongo.
Akizungumza mbele ya Kamati hiyo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis alisema Wizara itatekeleza maelekezo ya Kamati na zaidi itahakikisha malengo ya kuboresha elimu yanafikiwa.
Naibu Waziri Mwanaidi alisema, Kamati hiyo ina mchango mkubwa katika kusukuma mbele mipango ya Wizara ikiwemo uboreshaji wa miundombinu vyuo vya maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii.
Katibu Mkuu wa Wizara Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema Juhudi za kuboresha mazingira ya Vyuo vinavyosimamiwa na Wizara zimeanza.
"Waheshimiwa Wabunge kama mnavyoelewa, hii ni Wizara mpya ambayo timekabidhiwa tarehe 10 Januari, nasi tumeanza kutafuta mbinu za kutafuta ufumbuzi matatizo mbalimbali. Lakini tunashukuru kwamba mmejionea hali ilivyo tutaendelea kutembea pamoja kuleta mabadiliko" alisema.
Awali akiwasilisha taarifa, Mkuu wa Chuo cha Rungemba, Kidubya Kulamiwa alisema Chuo kimeanza kufanya ukarabati wa miundombinu ya ikiwemo jengo la Utawala na Jengo la uokaji.
Kulamiwa alisema sambamba na hatua za ukarabati, Chuo kinaendesha miradi ya kilimo cha ufugaji wa nyuki, parachichi, ufugaji wa Samaki na mradi wa Uokaji mikate na kusindika bidhaa zinazotokana na mazao ili kuboresha lishe hasa kwa wakazi wa Mkoa wa Iringa.
0 Comments