MKUU wa wilaya ya Kibaha Sara Msafiri amesema eneo la viwanda la Zegereni litawekewa miundombinu yote inayohitajika ili kuwaondolea changamoto wawekezaji wa viwanda.
Msafiri aliyasema hayo alipotembelea eneo hilo la viwanda kujua changamoto zilizopo kwenye eneo hilo.
Alisema kuwa miundombinu hiyo ni pamoja na ile ya umeme ambapo kutakuwa umeme wa viwanda pekee kwenye eneo hilo kwani uliopo hauna nguvu ya kutosha.
Alisema kuwa miundombinu mingine ni bomba maalumu la maji na barabara kiwango cha lami ambapo kwa sasa imewekwa sehemu ndogo.
"Lengo ni mazingira ya uwekezaji kwenye eneo hili ambalo limetengwa maalumu na Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa ajili ya viwanda ambalo lilikuwa bado halijakamilika kimiundombinu,"alisema Msafiri.
Kwa upande wa ofisa rasilimali watu wa kiwanda cha mabomba ya chuma Jafra Investment Supplies Company LTD Metsedeck Piason alisema kuwa kiwanda hicho kinazalisha tani 40 kwa siku.
Naye Prosper Ernest wa kiwanda cha BNBM Building Materials kinachojihusisha na utengenezaji wa marumaru alisema kuwa changamoto kubwa ni bidhaa za aina hiyo kuingizwa nchini na kuwafanya soko lao kuwa dogo.
0 Comments