Teddy Kilanga _Arusha
Waziri wa maendeleo ya jamii,jinsia,wanawake na makundi maalum,Dkt.Dorothy Gwajima anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku wanawake duniani mnamo machi 8,2022.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongella alisema sambamba na kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo pia atazindua kanzi data ya wanawake na uongozi Tanzania.
Aidha Mongella alisema wanapoelekea katika kilele cha maadhimisho hayo Ofisi yake kwa kushirikiana na wizara ya maendeleo ya jamii,jinsia,wanawake na watu wenye makundi maalum pamoja na Taasisi za kijamii nchini wataungana na wanawake wa mkoa huo katika kufanikisha zoezi hilo.
"Ratiba ya Maadhimisho haya kuanzia lmachi 4,2022 wanawake watatembelea wodi za akinamama katika hospitali ya Levolosi ambapo watafanya usafi na kutoa msaada wa vifaa mbalimbali katika wodi ya wazazi,"alisema Mongella.
Mongella alisema machi 5 mwaka huu wanawake wote wa mkoa wa Arusha watapata fursa ya kutembelea mbuga za wanyama Ngorongoro ambapo mgeni rasmi atakuwa Naibu waziri wa maliasili na utalii,Mary Francis.
Alisema machi 6 wanawake wa mkoa huoa watakuwa na mbio za kilometa 5 hadi 10 ambapo wanatazamia kuongozwa na Naibu waziri wa Utamaduni, sanaa na michezo Poul Gekul ikiwa machi 7,2022 kutakuwa na kongamano la wanawake takribani 300 ambapo litaendesha na chuo cha maendeleo ya jamii,jinsia ,wanawake na makundi maalum.
"Na kuanzia machi 6 hadi 8 mwaka huukutakuwa na maonesho mbalimbali ya watoa huduma za wanawake na jamii pamoja na wajasiriamali kuuza na kuonesha bidhaa zao ambapo uzinduzi wa maonesho haya yatazinduliwa na mimi mwenye mnamo machi 7,2022,"alisema Mongella.
Naye Afisa maendeleo wa mkoa wa Arusha,Blandina Nkini alisema anawaomba wanawake wajitokeze ili waweze kuadhimisha siku yao ambayo itakuwa sehemu ya kubadilishana mawazo pia kutakuwa na zawadi mbalimbali kama medali.
Nkini alisema katika maadhimisho hayo watakuwa na sare za kanga zenye sura ya Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan.
"Tunawakaribisha wanawake na jamiii ya wanaArusha kutoka sehemu mbalimbali kufika katika maadhimisho hayo ikiwa kauli mbiu ni HAKI SAWA KWA MAENDELEO ENDELEVU KUJITOKEZA KUHESABIWA,"alisema Nkini.
0 Comments