Header Ads Widget

BREAKING:ASKOFU KKKT DAYOSISI YA KONDE DR MWAIKALE AVULIWA UONGOZI YEYE AGOMA


Mkutano mkuu maalumu wa Dayosisi ya Konde ulioitishwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo umemvua wadhifa wa uaskofu, Askofu wa dayosisi hiyo, Edward Mwaikali na kuibua maswali.

Wajumbe wa mkutano huo ambao walikuwa ni wale waliohudhuria mkutano mkuu wa dayosisi hiyo mwaka 2017, pia walimchagua kwa kura 2,014, Mchungaji Geofrey Mwakihaba kuwa Askofu mteule wa dayosisi hiyo ya Konde.


Mbali na kumuondoa madarakani Askofu Mwaikali, tume iliyoundwa na mkuu wa kanisa chini ya uenyekiti wa Askofu Alex Malasusa, imerejesha makao makuu ya dayosisi hiyo Tukuyu kutoka Ruanda jijini Mbeya huku utaratibu wa kurudisha kiti cha askofu ukiandaliwa.


Hata hivyo, akizungumza na Matukio Daima Media kwa simu, Askofu Mwaikali alipinga uamuzi huo akisema utaratibu uliotumika haupo mahali popote pale na kwamba zipo taratibu za kikatiba za kumuondoa askofu lakini hazikufuatwa.


“Mimi sikuhudhuria huo mkutano kwa sababu nilikuwa siutambui na hili nilishalisema tangu mwanzo.Nimesikia tu kwamba maamuzi ni hayo, sijaambiwa rasmi. Wakishaniambia nitakuwa na neno la kusema,” alisema Askofu Mwaikali.


“Kimsingi mkuu wa Kanisa la KKKT amewatwisha laana wana Dayosisi ya Konde kwa sababu amekwepa kuwa mwenyekiti wa mkutano aliouitisha mwenyewe bila kushirikisha Halmashauri Kuu ya KKKT Konde. Amenawa mikono kama alivyofanya Pilato.


“Wajumbe wa huo mkutano hawakuwa halali kwa sababu Katiba ya KKKT Dayosisi ya Konde kanuni ya 06.29.03.01 inasema hakutakuwa na kipindi maalumu cha ujumbe wa mkutano mkuu,” alisema Askofu Mwaikali na kuongeza kuwa:


“Mkuu wa Kanisa katika barua yake aliagiza kwamba wajumbe watakaoshiriki mkutano mkuu ni wale wa mkutano mkuu wa 2017, si sawa hata kidogo,” alisema.


Uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya dayosisi hiyo kutoka Tukuyu kwenda Usharika wa Ruanda jijini Mbeya unaelezwa kupata baraka za mkutano mkuu wa dayosisi ambapo kura 202 ziliafiki uhamisho huo na kura mbili zilikataa.


Hata hivyo, uamuzi huo haukuafikiwa na baadhi ya wachungaji na waumini wa dayosisi hiyo, hususan wa Tukuyu, na hapo ndipo mgogoro ulipoibuka na tume ya Askofu Malasusa iliyoundwa kuchunguza, ilisema uamuzi huo ulikiuka katiba ya Dayosisi ya Konde. Baada ya jitihada za kusuluhisha mgogoro huo kushindikana kwa zaidi ya mwaka, mkuu wa Kanisa aliingilia kati na kuitisha mkutano mkuu maalumu juzi, ambao umemuondoa Askofu Mwaikali.

Ahsante Kwa kuchagua Matukio Daima blog ,Karibu Sana ujiunge na familia ya Matukio Daima Media Kwa kupakua APP ya Matukio Daima kupitia Google Play store ni bure kabisa kupitia App hii utaweza kuunganishwa na habari zinazotolewa na media zetu ikiwemo blog , Instagram, Twitter na Online Tv karibu Sana pia Kwa huduma ya matangazo na habari wasiliana nasi Kwa simu 0754 026 299


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI