Na WAF – Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka wataalam wa afya mazingira katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya umuhimu wa kupanda miti na kusafisha mazingira ili kuepusha jamii na magonjwa ya kuambukiza.
Dkt. Mollel amesema hayo mapema leo wakati akiongea na Wananchi katika soko la Mavunde (Soko la Chang'ombe) baada ya kufanya usafi katika eneo hilo ikiwa ni sehemu ya zoezi endelevu la kuhamasisha Wananchi kufanya usafi wa mazingira na kupanda miti.
"Sasa tunataka wataalam wetu wa Halmashauri na Mkoa muweke nguvu katika kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kutunza mazingira pamoja na kupanda miti” amesema Dkt. Mollel na kusisitiza Wataalam hao kuhakikisha wanasimamia angalau kila mtu apande walau miti 20 kwa mwaka huku akisisitiza zoezi hilo liende mpaka kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Aidha Dkt .Mollel amewahamasisha pia wananchi wa Dodoma kujenga utamaduni wa kupanda miti katika maeneo yao ya kuishi na maeneo wanayofanyia shughuli za kukuza uchumi ili kutunza mazingira na kupendezesha mji.
Dkt. Mollel amesema moja kati ya visababishi vya kuongeza umri wa kuishi ni pamoja na kufanya usafi wa mazingira yetu ili kuzuia milipuko ya magonjwa kama vile Kipindupindu yanayoweza kupelekea kupoteza maisha kwa wananchi ambao hawafuati kanuni za usafi wa mazingira.
"Nawashukuru sana Watendaji mnaofanya kazi hii, mkifanya mazingira yenu kuwa mazuri gharama ya kusafisha mazingira ni kidogo kuliko gharama ya kwenda hospitali kwaajili ya kutibu magonjwa yanayotokana na mazingira yetu kuwa machafu"
ameshukuru Dkt. Mollel.
Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Bi. Mary Maganga amesema, katika kuelekea uzinduzi wa Sera ya Taifa ya mazingira Mwaka 2021, Wizara yake kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) imeanza zoezi la kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma ikiwq ni sehemu ya kutunza mazingira.
Ameendelea kusema kuwa, shughuli ya upandaji miti imeenda sambamba na shughuli ya usafi wa mazingira, ambapo leo Februari 10, 2021 Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imefanya usafi katika eneo la soko la Mavunde (Soko la Chang'ombe) kama sehemu ya kuhamasisha wananchi kufanya usafi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Soko la Mavunde Bw. Godfrey Mbilinyi ameishukuru Serikali kwa kuchagua kufanya usafi katika Soko hilo, kwani itaamsha hali kwa wafanyabiashara na wakazi wa Chang'ombe kufanya usafi na kupanda miti.
0 Comments