Header Ads Widget

WASAMBAA MTANI UGAWA MALI ZA MAREHEMU

 


Adeladius Makwega-DODOMA.


Asili ya kabila ya Wasambaa inaaminika kuwa ni kutoka kundi la makabila linalofahamika kama WAKINASEUTA kundi hili linajumuisha Wabondei, Wazigua na Washambala. Watu wote hawa walifika Handeni wakitokea huko Kenya. Walipofika Handeni walikutana na wenyeji wa asili wa Handeni ambao walikuwa ni Wamasai.


Wamasai walipoona kundi la wageni limefika katika ardhi hiyo walitambua kuwa sasa wameingiliwa na wageni pengine hao wamekuja kuwapokonya ardhi yao, kwa uamuzi wao wa haraka ulikuwa ni kupambana nao kufa na kupona na si vinginevyo. Mapigano haya yalisababisha baadhi ya WAKINASEUTA kukimbilia kwenye Safu ya Milima ya Usambara na wengine kukimbili bondeni yaani Bondei.


Wengine walijaribu kupambana na Wamasai hao na wao kubakia Handeni. Hawa waliokimbilia Usambara milimani walikutana na wenyeji wa Usambaani wa asili waliokuwa wakifahamika kama WAKINATUI. WAKINASEUTA hao  narudia kukwambia kuwa ni Wasambaa, Wabondei na Wazigua walikuwa wakiabudu pamoja, hii  ikimaanisha ni kundi moja la watu.


“Seuta mziuwa ne ngone ntongo, tiase nkoba na mungu.” 


Hapa wakimaanisha kuwa WAKINASEUTA mmekufa lakini kumbukeni kuwa sie mmetuacha hapa. mtukumbuke huku mlipotuacha. Maneno haya yalikuwa yakisemwa katika matambiko yao.


Utani ndani ya kabila hili unatazamwa tangu WAKINATUI walipowapokea WAKINASEUTA wakitokea huko Handeni.


Kwa kuwa WAKINATUI walipambana na WAKINASEUTA, hapo utani huibuka.


“Inyi nuwa vyee du.”

Hapa kinachofananaishwa ni kuwa (Hashakumu si matusi) WAKINASEUTA wote ni wanawake. Jambo hilo mwanzoni lilileta maneno mno huku WAKINASEUTA wakishindwa kuvumilia.


Je wanafanyaje? Wanarudi Handeni au wanarudi Kenya? Hapo WAKINASEUTA kurudi Handeni walishindwa wakihofia Wamasai na kurudi Kenya walikuwa wametoka miaka mingi. Walibaki njia panda.


Kwa hekima walipatana na WAKINATUI na hilo likasaidia wao kubaki usambaani hadi leo, mapatano hayo ndiyo yakaleta utani baina yao.


Walianza kuoleana na hapo ukawa udugu mkubwa wa baina yao na jambo hilo likawafanya hadi leo ni vigumu kuwatafautisha ndugu hawa wawili.


Utani ulikuwa mkubwa mno, huku ukiwa na nia ya kuchekeshana na hata kusumbuana ilimradi mtu aone mwezake anasumbuka kwa utania huo. Kwa mfano Hamisi ambaye ni WAKINASEUTA aliyeoa kwa akina Juma ambao ni WAKINATUI wakati wa msiba wanaweza kutaniana vizuri sana bila woga.


Ndugu A.J Mshihiri katika mojawapo ya kazi zake juu ya utani wa kabila la Wasambaa anasema kuwa mwishoni mwa mwaka 1969 alikwenda kwao huko Mgwashi-Lushoto Tanga alipofika huko ulitokea msiba ambapo mama mmoja alipata ujauzitio kutoka kwa mwanaume mwingine ambaye hakuwa mumewe. Kutokana na fedhea hiyo mwanamke huyu alikuwa akitafuta njia ya kuepukana na balaa hilo.


Mwanamke huyu alikuwa akifanya kazi ya Uganga wa Kienyeji, alipofariki katika harakati hizo za kuficha fedhea ya mimba hiyo. 


Wanakijiji cha Mgwashi walidai kuwa kutokana na kupata ujauzito huo aliamua kujiroga mwenyewe afae ili kuficha fedhea ya mimba hiyo ya mwanaume mwingine. Kwa mujibu wa maelezo ya ndugu A.J. Mshihiri ambaye alikuwepo siku ya tukio hilo anadai kuwa alibaini kuwa marehemu huyo alikuwa ni MKINASEUTA.


Miongoni mwa watani aliyefanya vibwanga ni Shemukai ambaye yeye kiasili alikuwa ni MKINATUI.


Shemukai alipofika hapo alitoa maneno mengi machafu juu ya marehemu huyo ambaye kwa kisambaa maiti inaitwa “Namsi.” Shemukai alifanya vurugu kubwa.


“Huyu marehemu alikuwa mshenzi sana, hakuwa na rafiki na ni mtu mkorofi mno , ni mchawi. Huku alikuwa anajidai sana. Tunashukuru sana kwa kuwa alikuwa na sifa mbaya zote hizo, ni heri amekuwa miongoni mwa wafu na si miongoni mwa tuliohai.”


Maneno haya japokuwa yalikuwa makali yalichukuliwa kama utani tu na ndugu wa marehemu waliendelea kulia tu kwa kumpoteza ndugu yao. Shemukai alifika hadi ndani ya nyumba ya ndugu wa marehemu.


“Ebu  nyie nyamazeni mmempoteza kuku tu.”


WAKINASEUTA hilo halikuwa neno, walizika salama ndugu yao wakishirikiana na WAKINATUI na hadi msiba ukaisha salama salimini


Jambo la kustajabisha kwa Wasambaa panapotokei msiba, mtani ndiye mwenye jukumu la kugawa mali za marehemu. Mtani akiwa katika zoezi hilo yeye anaweza kuchukua nguo moja au mbili za marehemu na mara nyingi huwa vitu vidogovidogo.


Kwa kuwa Wasambaa wana tabia ya kurithishana wake, mtani ndiye mtu mwenye nafasi ya kumuuliza mke wa marehemu kama anataka kulithiwa na nani? Kati ya wadogo wa marehemu.


Hapo mwanakwetu mashemeji wanatakiwa kukaa vizuri sana na mke wa kaka yao maana akifa kaka, shemeji hawezi kukuchagua kama ulikuwa unamsumbua.


Jina la aliyechaguliwa atapatiwa mtani na mjane na mjane huyo atamalizi sehemu ya maisha yaliyobaki na mume mpya ambaye alikuwa ni mdogo au kaka wa marehemu.


Kwa wasambaa utani si wakati wa misiba tu unaweza kufanyika wakati wowote ule. Haya nayaweka kiporo msomaji wa matini hizi.Lakini kumbuka kuwa haya ninayasema kwa tahadhari sana maana nisije nikarudi Usambaani nikapokonywa mke kisa nimetoa siri za Wasambaa katika matini zangu.


Je kipi kitaendelea katika utani wa kabila hili?


Subiri matini ijayo.


Nakutakia siku njema.


makwadeldius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI