Header Ads Widget

WAZIRI WA AFYA; ATOA WITO KWA WANAWAKE KUHAKIKISHA USAFI ,MATUMIZI YA BIDHAA SALAMA.

 

Na Hamida Ramadhan,Matukio.Daima App Dodoma

WAZIRI wa Afya, Janestar Mhagama, amesema kuwa ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza (Non-Communicable Diseases - NCDs) kama vile kisukari, shinikizo la damu, na matatizo ya figo, limeendelea kuwa changamoto kubwa kwa serikali kutokana na gharama kubwa za matibabu zinazohitajika kuyakabili.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa kwa wakina mama na watoto vilivyotolewa na kampuni ya Doweicar technology company  LTD Waziri Mhagama alieleza kuwa magonjwa hayo si tu yanatishia ustawi wa jamii bali pia yanachangia kwa kiasi kikubwa matumizi makubwa ya rasilimali za serikali kwenye sekta ya afya.

"Ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza linazidi kuongeza mzigo kwa serikali. Hali hii inatufanya tuimarishe zaidi juhudi za kinga na kuhimiza wananchi kuchukua hatua za mapema za kujilinda na magonjwa haya," amesema Mhagama.


Katika kuimarisha afya ya wanawake, Waziri huyo amewataka akinamama  hususan walioko katika hedhi au waliokwisha jifungua  kuwa makini na bidhaa wanazotumia, akisisitiza umuhimu wa kutumia bidhaa zilizoidhinishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuepuka maambukizi hatarishi.

Ameeleza kuwa matumizi ya bidhaa zisizokidhi viwango yanaweza kusababisha maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), ambayo huweza kusababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuathiri figo.

“Napenda kuwasihi akinamama kutumia bidhaa bora na salama kama vile pedi za SOFTCARE ambazo zimethibitishwa na TBS. Bidhaa hizi siyo tu zina viwango bali pia zinasaidia kupunguza hatari ya kupata UTI, ambayo ikiambatana na kuchelewa kutibiwa, inaweza kusababisha matatizo ya figo,” alisema Waziri.

Aidha, ametoa rai kwa wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kuendelea kuelimishana juu ya umuhimu wa usafi wa mwili, hasa kwa wanawake na wasichana, ili kuhakikisha taifa lina kizazi chenye afya bora.

Kwa upande wake, Balozi wa Softcare, Zari The Boss Lady,  amewasihi kina mama kuendelea kutumia pedi za kampuni hiyo kwani zimetengenezwa kwa pamba halisi na ni rafiki kwa mama awapo kwenye siku zake. Kwa watoto wadogo pia ni rafiki na hazichubui, hivyo kumfanya mtoto kuwa huru wakati wote.

"Pedi hizi ni nzuri na ni rafiki wa mazingira hivyo, nawasihi kina mama wenzangu kuifanya kuwa chaguo lao la kwanza, kwani hazichubui na ni salama kwa afya ya kila mwanamke anapokuwa kwenye siku zake, na salama zaidi kwa watoto," amesema Zari.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema anawashukuru Softcare kwa kuweza kuwafikia kina mama wa Mkoa wa Dodoma, na amefurahishwa kujua kuwa kampuni hiyo imethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na kwamba bidhaa zake ni nzuri kwa kina mama na watoto bila kuleta madhara ya kiafya. 

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI