WAFANYAKAZI mkoani Pwani wametakiwa kutoa taarifa endapo kwa baadhi ya waajiri ambao wanakiuka mikataba ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwanyima stahiki zao ikiwa ni pamoja na hali bora za kazi.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na katibu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Viwanda Biashara Taasisi za Fedha Huduma na Ushauri (TUICO) mkoa wa Pwani Neema Wilbard alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Wilbard alisema kuwa kazi yao kubwa ni kulinda na kutetea maslahi ya wafanayakazi sehemu za kazi ili mikataba waliyoingia na waajiri ifuatwe na kuwatetea pale wanapodhulumiwa stahiki zake zilizopo kisheria.
"Moja ya kazi za chama inachokifanya ni kumshauri mwajiri ili kumwekea mfanyakazi hali bora ya kazi ambapo mkataba wake unamnufaisha mfanyakazi na maslahi yake,"alisema Wilbard.
Alisema kuwa mkataba wa hali bora unatetea wafanyakazi kwani unazungumzia haki unaboresha na kile ambapo hakipo ili akipate ikiwa kipo kiongezeke.
"Kingine ni kuongeza mshahara, nauli na kama ipo iongezwe, chakula, likizo na matibabu na baadhi ya vitu ambavyo havipo hata kwenye sheria ambapo huu ni moja ya mikataba mizuri japo iko mingi,"alisema Wilbard.
Aidha alisema kuwa kazi nyingine ya chama ni kufanya utetezi pale waajiri wanapokuwa wamekwenda kinyume na mikataba ikiwa ni pamoja na kukiuka mikataba ya kazi ambayo iko kisheria.
0 Comments