Kijiji cha Mkelezanga kilikuwa kipo katika Kata ya Mkamba ambapo ni jirani na Barabara inayoenda Kilwa. Hapa ni kwa ndani kidogo kwa kupitia Kijiji cha Kimanzichama, Wilayani Kisarawe (Mkuranga kwa sasa), Mkoa wa Pwani. Kwa wakati huo nadhani ilikuwa kati ya miaka ya 1980s.......ADELADIUS MAKWEGA_DODOMA.
Kijiji hiki kilikuwa na nyumba za wanakijiji za mbavu za mbwa karibu zote na kulikuwa na shule ya Msingi Mkelezange ambayo nayo ilikuwa sawa na nyumba za wanakijiji huku juu wakiezeka makuti aina viungo. Shule hii ilikuwa na madarsa manne na nyumba mbili za walimu ambazo hazikuwa za bati pia.
Madhari ya kijiji hicho ilikuwa ya minazi mingi, michungwa, ndimu za kutosha na hata pale tulipokuwa tunakaa ilikuwa ni jambo lakuzunguka uani tu na kuchuma ndimu wakati mbogo ikichemka mekoni. Katika nyumba hizi mbili za walimu walikaa walimu watatu Mwalimu John Kiondo huyu alikuwa ni mzaliwa Tanga na Mwalimu Francis Makwega na Mwalimu Doroth Mlemeta (hawa wawili ndiyo wazazi wangu).
Nakumbuka tukiwa pele Mkelezange ununuzi wa Orange Skwashi hakukuwepo kwa kuwa ukamuaji wa ndimu na kuwekewa sukari na kunywa ilikuwa ikifanyika kila mara, kwani ndimu zilikuwa zikiiva hadi kuwa za njano na kuanguka chini.
“Kanichumie ndimu, usiokote za chini, chuma iliyopo katika mti.” Haya yalikuwa maagizo ya kawaida ya mama yangu tukiwa hapo, Mkelezange.
Mwalimu John Kiondo huyu alikuwa akitokea Kwemaramba-Muheza (Sasa ni Mkinga)-Tanga, Mwalimu Francis Makwega akitokea Kilindoni -Mafia na Mwalimu Doroth Mlemeta akitokea Kilimatinde Singida-huyu akiwa mke wa mwalimu Makwega. Huyu mwalimu wa Muheza na huyu wa Mafia mazingira ya Mkelezanga hayakuwa mageni kwao kwani yote yalikuwa ni mazingira ya Pwani.
Nadhani Profesa Kighoma Malima alikuwa msomi na mwalimu aliyefundisha vyuo vikuu ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri awali aliyafahamu fika mazingira ya kwao, kwa hiyo lazima palikuwa na shinikizo la watumishi wanaopelekwa kwao wawe watu wanaolewa mazingira ya pwani kwa kiasi. Wahusika wa elimu wa wakati huo walikuwa wakimpanga mtumishi kufanya kazi au kuhamia walikuwa wanatazama je mazingira hayo yatalinga na alipozaliwa/alipokulia? Huyu mwalimu Makwega alikuwa akihamia hapo na mkewe wakitokea Mpwapwa kurudi nyumbani, ndiyo akapangiwa Mkelezange.
Kijiji hiki hakikuwa na zahanati wala huduma nyengine yoyote ya afya bali huduma zote za afya zilikuwa zikifanyika katani Mkamba. Nakumbuka hata wanafunzi waliokuwa wakiumwa wanafika shuleni wanaomba ruhusa wanakwenda kutibiwa huko Mkamba ambapo ulikuwa ni mwendo mrefu kidogo. Kwa wakati huo nadhani Mkamba ilikuwa kama Kituo cha Afya, huku vijiji vingine kama Kilimahewa na Kimanzichana, wanapokuwa na wagonjwa au kina mama kujifungua walikuwa wakikaribia kujifungua walihamia jirani na kituo hiki cha afya au kwenda kujifungulia Temeke Hospitali-Dar es Salaam.
Nakumbuka hili hata mama yangu mzazi katika kipindi hicho alizaliwa mdogo wangu wa mwisho kweli ilibidi mama kwenda kujisikilizia Dar es Salaam na baadaye akajifungulia Temeke Hospitali.
Wengine walikuwa wakifika Dar es Salaam wanapanga vyumba, wengine wanakaa kwa ndugu zao hadi uchungu ukifika ndipo anapelekwa Temeke kujifungulia lakini katika vijiji hivyo wengi walikuwa wakijifungulia majumbani kwa wakunga wa jadi.
Mbunge wa Jimbo la Kisarawe wakati huo alikuwa ni msomi huyu Profesa Kighoma Malima ambaye ndiye aliyesaidia sana ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mkamba ambapo huko ndipo kulikuwa kwao kwa kuzaliwa kabisa. Nakumbuka alikuwa akifika na kuwatembelea walimu na kuzungumza nao huku akiwa amevalia kombati za kaki akikagua maendeleo ya shule zake.
Mahusiano ya watu wa vijiji hivi na Dar es Salaam yalikuwa makubwa sana, iwe ndoa sherehe na misiba huku usafirishaji wa ndizi, embe ndimu, nazi ilikuwa ni desturi. Nakumbuka walikuwa wakivuna mikungu ya ndizi, wakichimba shimo na kuizika kwa kuifunika kwa majani, alafu wanachimba shimo dogo kuelekea kwenye shimo kubwa huku wakiwasha moto na kuupuliza moshi kuiingia katika shimo kubwa lenye ndizi. Ndizi hizo zilikuwa zinakaa shimoni kwa siku mbili alafu zinatolewa zinakuwa zimeanza kuiva na kuzisafirisha hadi sokoni Dar es Salaam kuuzwa, huku wakisema kuwa tendo hilo ni kuzipepea.
Mwezi wa 12 ni wakati ambapo korosho huwa zinavunwa sana huku watoto wa eneo hili tulikuwa bize na kuucheza mchezo unaofahamika kama Kisago(Sago) ambapo ni kama kamali ya korosho. Baba yangu alitujulisha kuwa kesho tunaanza safari ya kwenda Mbagala Dar es Salaam kwenda kula sikukuu ya Krisimasi. Jambo hilo lilinikwaza sana maana harakati za mchezo wa Kisago zilikuwa zimepamba moto mno lakini mkuu wa kaya kasema, hapo hakuna budi. Nilichokifanya nilichukua korosho zangu za kuchezea kisago na kuzichoma na kula na wezangu kwa kuwa sasa michezo ya mjini si michezo vijijini na michezo ya vijijini si ya mjini.
Nilimuuliza mama inakuwaje tunafunga safari hadi huko alinjibu kuwa hapo hakuna Kanisa bali safari hadi Dar es Salaam ili tuwahi kuzaliwa pamoja na Bwana ambapo ndipo kulikuwa na Kanisa Katoliki huku eneo hilo la Mkamba likiwa sehemu ya Parokia ya Mbagala.
Kwa utaratibu wa safari tuliondoka Mkelezange jioni ya siku hiyo na kufika Kimanzichana na kulala katika basi. Kimanzichana ya wakati huo ilikuwa ni Kijiji cha Ujamaa chenye nyumba kadhaa bora za bati huku kukiwa na nyumba moja iliyokuwa kama ghorofa ambayo nakumbuka walisema ni mali ya tajiri mmoja aliyefahamika kama Kipende. Palikuwa na lori moja kuukuu la Bedford ambao lilikuwa bovu ikiaminika kuwa lilikuwa mali ya kijiji hicho.
“Lori hili lilikuwa linafanya kazi kama ile Isuzu Direct Injection ya Kijiji cha Ujamaa Mkiu, sema liliharibika tukashindwa kulitengeneza. Kijiji chetu kilikuwa hadi na maduka.”
Baadhi ya wanakijiji walikuwa wakitusimulia siye washamba tuliokuwa tunatokea huko Mkelezanga, lakini nyumbani kwa Mbunge msomi Profesa Kighoma Malima ambaye ni Baba Mzazi wa Adam Malima ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa sasa.
Kimanzichana palikuwa na magenge mengi ya biashara wikifanyika biashara saa 24 wakati huo. Hapa pia walikuwa na shule ya msingi moja nzuri ya bati. Huku ikisemekana kuwa eneo hilo lilikuwa la wajanja.
“Kimanzichana usije mchana, ukija mchana tutakuchana, ukija usiku tutakuvizia.”
Hayo yalikuwa maneno ya magangwe wa eneo hilo wakati huo.
Alfajiri ndipo safari ya kwenda Mbagala ilianza, Japokuwa safari ilianza asubuhi huku tukipita katika vijiji vingi hali yake ilikuwa duni eneo ambalo lilikuwa na maduka na nyumba nyingi za bati ilikuwa ni Mkuranga ambalo lilikuwa linakaribiana kimaendeleo na Kimazichana.
Tukiwa katika basi hilo abiria wakisimulia kuwa Mkuranga ilitakiwa kuwa Wilaya tangu Mkoloni kwa kuwa lilikuwa eneo la katikati kwa Wilaya ya Kisarawe. Mimi nikiwa sifahamu hata wilaya wakati huo maana yake nini.
Tulipofika Mbagala tulishuka pahala ambapo ni kituo cha Mbagala 77 kulikuwa na Bar moja kubwa maarufu ambayo ilifahamika kama 77 Bar ambayo nadhani ndiyo iliyoipa jina eneo hilo la Mbagala 77. Muda huo ilikuwa saa nane ikiwa safari ndefu sana kutokana na ubovu wa barabara na aina ya magari ya wakati huo. Tukifika salama safari yetu ya kutoka Mkelezange kwenda Mbagala.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments